Na Lucy Lyatuu, Dodoma
TUME ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imeshauriwa kutoa Elimu ya Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuanzia ngazi ya Shule za msingi ili kuwa na jamii inayoheshimu faragha na Taarifa Binafsi za watu.
Ushauri huo umetolewa leo Juni 21, 2026 jijini Dodoma na Bw. Fred Nyandoro, Mkazi wa Dodoma alipotembelea banda la PDPC lililopo kwenye viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma na kupata elimu ya Dhana ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kutoka kwa wataalamu wa PDPC.
“Ushauri wangu kwa Tume ni vizuri kuaanza kutoa elimu kuanzia ngazi ya Shule za awali, msingi, sekondari na vyuo kwa kuwa tukiwajengea vijana uwezo wa kutambua na kuelewa umuhimu wa ulinzi wa Taarifa hasa Taarifa Binafsi tutaendelea kuwa na jamii ambayo inajitambua na inayoheshimu Faragha na Taarifa Binafsi za watu. Pia naishauri jamii kwa ujumla kuhakikisha Taarifa zetu zinakua ni za siri” amesema Bw. Nyandoro
PDPC imeweka kambi ya siku nane (8) kuanzia Juni 16,2026 mpaka Juni 23, 2026 kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, 2026, yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma ili kutoa huduma mbalimbali za PDPC, ikiwemo Elimu na Ushauri kuhusu Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44 (PDPA) kwa wananchi na watumishi wa umma.

