Na Lucy Lyatuu,Dodoma
TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI)
imesema imefanikiwa kupunguza kwa asilimia 98 rufaa za wagonjwa wa mifupa na asilimia 97 kwa wagonjwa wenye changamoto za ubongo, kufuatia kuanzishwa na kuimarishwa kwa huduma mbalimbali za kibingwa na ubingwa bobezi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema hayo leo Septemba 1, 2026, jijini Dodoma wakati akieleza mafanikio ya Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja, kuanzia Julai 2025 hadi Juni 2026.
Amesema katika kipindi hicho MOI imeendelea kuboresha huduma kwa kuanzisha na kuimarisha matibabu ya kisasa, ikiwemo upasuaji wa ubongo kwa kutumia akili unde, uchukuaji wa sampuli za vipimo kwa njia ya matundu, tiba ya maumivu, upasuaji rekebishi wa viungo vilivyopooza, upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia tundu la pua pamoja na upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu.
Dkt. Ulisubisya, amesema huduma nyingine zilizoimarishwa ni pamoja na matibabu ya maumivu sugu ya mgongo, kuweka tiba simenti kwenye pingili za mgongo zilizovunjika, mfumo wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao na huduma ya kutibu kiharusi.
Amesema hatua hiyo imeongeza uwezo wa MOI kutoa huduma ambazo awali wagonjwa walilazimika kupewa rufaa nje ya nchi, ambapo katika mwaka huo wagonjwa 2,282 walipatiwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa mafanikio, hatua iliyoiwezesha Serikali kuokoa Shilingi bilioni 121.99 ambazo zingetumika endapo wagonjwa hao wangetibiwa nje ya nchi.
Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, MOI ilihudumia jumla ya wagonjwa 211,359, ambapo wagonjwa 202,000 walipata huduma za wagonjwa wa nje (OPD), huku wagonjwa 9,359 wakilazwa kwa ajili ya matibabu.
Amesema ongezeko la huduma za kibingwa, wataalamu wenye uzoefu na matumizi ya teknolojia za kisasa pia limeifanya MOI kuwa miongoni mwa taasisi zinazovutia wagonjwa kutoka nje ya Tanzania kupitia huduma za tiba utalii.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2025/26 Taasisi imehudumia jumla ya wagonjwa 270 kutoka nchi za Comoro, Msumbiji, Malawi, Zambia, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Burundi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kadhalika amesema pia MOI imeimarisha hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi, ambapo utekelezaji wa mfumo huo umeongezeka kutoka asilimia 70 hadi asilimia 81, kupitia usafi wa mazingira, usafi wa mikono, matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga na kuzingatia taratibu salama za kuwahudumia wagonjwa.
Kuhusu tiba ya viungo, MOI imehudumia wagonjwa 71,819 katika kipindi hicho, huku huduma za mkoba zikifikia wagonjwa 18,455, ambapo 14,145 walipatiwa huduma za kliniki na 4,310 walifanyiwa upasuaji.
Dkt. Ulisubisya amesema katika kuimarisha rasilimali watu, MOI imewawezesha wataalamu saba kwenda masomoni nje ya nchi katika fani za ubingwa na ubingwa bobezi, huku watumishi 199 wakipandishwa vyeo, 15 wakibadilishiwa kada na watumishi 112 kuajiriwa.
Aidha, amesema ukarabati wa MOI Annex jijini Dar es Salaam wenye thamani ya Sh bilioni 2.1 umefikia asilimia 99 na unatarajiwa kuongeza uwezo wa Taasisi hiyo kuhudumia wagonjwa wa nje hadi kufikia wagonjwa 1,500 kwa siku.
Kuhusu maandalizi ya michuano ya AFCON 2027, Dkt. Ulisubisya amesema MOI imejipanga kutoa huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wanamichezo watakaoshiriki michuano hiyo, hususan katika kukabiliana na majeraha na changamoto nyingine za kiafya.
Amesema Taasisi ina zaidi ya madaktari bingwa bobezi sita waliobobea katika tiba za michezo, pamoja na kliniki maalum kwa wagonjwa wa kimataifa, vyumba 25 vya kisasa vya kulaza wagonjwa na vifaa vya kisasa vya uchunguzi na tiba.
Amesema Kitengo cha Dharura cha MOI pia kimeandaliwa kutoa huduma wakati wa michuano hiyo, huku akisisitiza kuwa Taasisi ipo tayari kuhudumia wanamichezo katika maeneo yatakayohusika na AFCON 2027, yakiwemo Zanzibar, Arusha na Dar es Salaam.

