Na Danson Kaijage
DODOMA:HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imeanzisha huduma ya kuvuna mifupa ya mbavu na nyonga kwa ajili ya kutengeneza taya ya chini ambapo gharama yake itakuwa Sh.Milioni 6.2.
Mkurugenzi huduma ya Upasuaji Muhimbili, Dkt.Rachel Mhavile amesema hayo wakati wa kutoa taarifa ya mafanikio kwa miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa waandishi wa habari katika ukumbi wa Habari Maelezo Jijini Dodoma.

Amesema huduma hiyo ni mpya katika hospitali za Umma nchini na itasaidia kuimarisha taya ya chini, mifupa hiyo itavunwa kwa mgonjwa mwenyewe baada ya kufanyiwa vipimo na kuona ni jinsi gani inafaa.
Akitoa ufafanuzi juu ya mifupa hiyo amesema kuwa mifupa itavunwa kwa mgonjwa mhusika anayetaka huduma ya kutibiwa taya na pindi atakapokuwa amepatiwa matibabu itakuwa moja kwa moja na siyo ya kutoa na kurejesha.
Pia amesema huduma hiyo itasaidia kutengeneza mizizi bandia ya meno ambayo nayo atawekewa mgonjwa , pia mgonjwa hatapata usumbufu wa kubadilisha mizizi hiyo au taya.
Akizungumzia suala la mafanikio kwa ajili ya watoto wanaozaliwa na tatizo ya kutosikia amesema kuwa Hospitali imeweza kuanzisha huduma ya upasuaji na kuweka vifaa vya kusaidia kusikia.
Amesema kwa sasa watoto 54 wamefanyiwa upasuaji na kuwekewa vifaa vya kuwasaidia kusikia kwa gharama ya Sh. bilioni 2.3 kwa wote na kusaidia kuokoa kiasi cha shilingi Bilioni nne kama wangeenda kutibiwa nje ya nchi.
Amesema huduma hiyo ya upasuaji kwa watoto ni kati ya watoto wa siku moja hadi miaka mitano ambao uchunguzwa na madakitari bingwa na bobezi ambao ni wazawa.