Na Danson Kaijage
DODOMA: SERIKALI kupitia bandari inatekeleza mapendekezo ya mpango kabambe ya maendeleo ya bandari nchini (2020 – 2045) na programu ya uboreshaji na uendeshaji wa bandari ambao ni mpango wa kitaifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Plasduce Mbossa amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari.
Amesema katika Programu hiyo bandari imejipanga kutekeleza miradi 10 ya kimkakati itakayoleta tija kwa taifa na kwa ustawi wa Bandari.
Miongoni mwa miradi hiyo ameitaja kuwa ni Mradi wa kupokelea na kuhifadhia mafuta, ambapo unagharimu dola za kimarekani million 265, na utekelezaji wake umefikia asilimia 17.
Amesema mradi huo ukikamilika utapunguza siku za kuhudumia meli zenye ujazo wa 150,000 DWT kutoka siku 10 mpaka tatu.
Mradi mwingine utagharimu dola za kimarekani milioni 119.9 ambao ni ujenzi wa kituo cha reli na mtandao wake ndani ya bandari ya Dar es Salaam.
“Mradi huu ukikamilika utapunguza kiwango cha asilimia 98 cha shehena inayotoka bandarini kwa kutumia njia ya barabara na kupelekea kutatua tatizo la msongamano wa malori ndani na nje ya bandari,” amesema.
Pia ameongeza kwamba, ujenzi wa gati mbili zenye jumla ya urefu wa mita 500, utagharimu dola za kimarekani million 250, kwamba ukikamilika utawezesha ufungaji wa meli mbili zenye ukubwa wa 50,000 DWT katika gati hizo kwa wakati mmoja.
Vile vile amesema mradi wa ujenzi wa bandari maalum ya kisiwa – mgao mkoani Mtwara kwa ajili ya kuhudumia shehena chafu, utagharimu dola za kimarekani milioni 171.
Maelezo yake ni kwamba, mradi huo umelenga kuepusha athari za kimazingira na kuondoa changamoto zinazotokana na kuhudumia mizigo katika bandari ya Mtwara.
Pia amesema uboreshaji wa gati namba nane hadi 11 yenye jumla za mita 720 pamoja na maeneo ya kuhifadhia makasha, utagharimu dola za kimarekani million 220.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa miradi mingine ni uendelezaji wa bandari kavu eneo la Kurasini na Ihumwa – Dodoma, itagharimu dola za kimarekani milioni 157.
Amesema mradi wa uendelezaji bandari ya Kigoma unagharimu dola za kimarekani milioni 48.82, unalenga kuimarisha uchumi wa ushoroba wa kati.
Vile vile ujenzi wa gati maalum la kuhudumia makasha na Gati la mafuta – Bandari ya Tanga utakaoghrimu dola za kimarekani milion 201.
“Ujenzi wa gati namba 12 hadi 15 utakao gharimu dola za kimarekani milion 591.564 unaolenga kuongeza ufanisi wa bandari ya DSM.
“Ujenzi wa bandari mpya ya Mbegani Bagamoyo utakao gharimu dola za kimarekani bilion 1.5.”amesema.