MFANYAKAZI TANZANIAMFANYAKAZI TANZANIA
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Search
Magazeti
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Habari Mpya
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Chagua hapa
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
  • Advertise
© 2024 Mfanyakazi Tanzania. All Rights Reserved.
Reading: Miaka 40 ya COSTECH: Teknolojia Yafungua Milango ya Elimu kwa Wasioona
Share
Notification Show More
Font ResizerAa
Font ResizerAa
MFANYAKAZI TANZANIAMFANYAKAZI TANZANIA
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Search
  • Home
  • Habari
  • Mfanyakazi
  • Magazeti
  • Bookmarks
Follow US
© 2022 Mfanyakazi Tanzania. All Rights Reserved.
MFANYAKAZI TANZANIA > Tovuti > Makala > Miaka 40 ya COSTECH: Teknolojia Yafungua Milango ya Elimu kwa Wasioona
Makala

Miaka 40 ya COSTECH: Teknolojia Yafungua Milango ya Elimu kwa Wasioona

Lucy Ngowi
By Lucy Ngowi
Share
9 Min Read
Na Lucy Ngowi
KWA mwanafunzi asiyeona, kitabu kinaweza kuwa zaidi ya kurasa zilizofungwa; kinaweza kuwa ukuta unaozuia maarifa.
Lakini kwa teknolojia inayobadilisha maandishi kuwa yanayoweza kusomeka kwa njia inayomfaa, ukuta huo unaanza kuporomoka na nafasi ya kujifunza inafunguka.
Hiyo ndiyo taswira inayojitokeza kupitia ubunifu wa Filbert Shio, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa kampuni ya Porto, ambaye ametengeneza teknolojia inayolenga kuwawezesha walimu na wanafunzi, wakiwamo wenye ulemavu wa macho, kushiriki kwa ufanisi zaidi katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.
Ubunifu huo unakuja wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 40 ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kipindi kinachotoa nafasi ya kutazama namna sayansi, teknolojia na ubunifu vinavyoweza kutoka kwenye mawazo ya wabunifu na kuwa suluhisho la changamoto zinazogusa maisha ya wananchi.
Kwa Mwalimu Alexina Masesa, anayefanya kazi katika Kiwanda cha kuchapisha vitabu kwa wasioona katika Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Dar es Salaam, yenye wanafunzi wenye ulemavu wa macho,
Anasema teknolojia hiyo si suala la ubunifu pekee; ni nyenzo inayoweza kuongeza ufanisi wa wanafunzi katika masomo na kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia kwa kujitegemea.
“Teknolojia ni nzuri, inasaidia wanafunzi kuifahamu teknolojia na aina mbalimbali za mashine kama vile skana na printer. Inaongeza uwezo kwa wasioona kuifahamu teknolojia ya Frakta,” anasema.
Habari Picha 13316
Teknolojia inayobadilisha uzoefu wa mwanafunzi
Kwa muda mrefu, changamoto ya upatikanaji wa nyenzo rafiki za kujifunzia imekuwa miongoni mwa vikwazo vinavyoweza kuathiri uzoefu wa wanafunzi wenye ulemavu wa macho.
Shio anasema mfumo wake umeundwa kuwakutanisha walimu na wanafunzi katika mazingira ya kidijitali, ambapo walimu wanaweza kuweka maudhui ya masomo, maswali na mitihani kwa ajili ya wanafunzi.
“Mfumo wetu unatumika kwa ajili ya walimu pamoja na wanafunzi, ambapo wanaweza kuwasiliana moja kwa moja. Walimu wanaweza kuweka maudhui mbalimbali ya masomo yote, maswali pamoja na mitihani,” anasema.
Kwa mwanafunzi asiyeona, thamani ya teknolojia hiyo ipo katika uwezo wa kupata maarifa kwa namna inayozingatia mahitaji yake.
Shio anaeleza kuwa vifaa vinavyohusishwa na mfumo huo vinaweza kumwezesha mwanafunzi kupata maudhui kwa njia ya kusikiliza na kushika, jambo linalolenga kuongeza uhuru wake katika kujifunza.
Hapo ndipo ubunifu unapovuka mipaka ya kifaa na kuingia katika maisha ya binadamu.
Mwanafunzi anapoweza kupata somo, kufanya kazi na kujifunza bila kutegemea msaada wa mtu mwingine kila wakati, teknolojia inakuwa nyenzo ya kumjengea kujiamini, kujitegemea na kushiriki zaidi katika elimu.
Mwalimu Alexina anaona fursa hiyo kwa upande wa wanafunzi anaowafundisha.
“Wanafunzi hiyo teknolojia itaongeza ufanisi katika masomo na pia kuongeza ubunifu na kufahamu teknolojia kwa undani zaidi,” anasema.
Kwa maelezo yake, wanafunzi wanapofahamu teknolojia hiyo wanapata msingi wa kutumia pia teknolojia nyingine, ikiwamo kompyuta.
Ubunifu unaogusa maisha
Shio anasema mfumo huo unalenga kutoa nafasi kwa wanafunzi kujifunza wakati wanaotaka, huku walimu nao wakiwa na uwezo wa kufundisha bila kuzuiwa na eneo.
“Teknolojia yetu inampa urahisi mwanafunzi kuweza kujitegemea na kujifunza wakati wote anapotaka. Mwalimu pia anaweza kufundisha popote pale anapotaka kwa sababu mfumo wetu unatumia intaneti,” anasema.
Mfumo huo pia unalenga kuwawezesha wanafunzi kuandaa kazi zao na kuwasiliana kwa njia ya barua pepe, pamoja na kutuma nyaraka au makala walizoandaa.
Habari Picha 13317
Matumizi ya Kiswahili na Kiingereza ni sehemu nyingine inayotajwa katika mfumo huo, jambo linaloweza kuwawezesha wanafunzi kutumia teknolojia kulingana na mazingira ya elimu wanayopitia.
Kwa mtazamo huo, teknolojia haibadilishi tu namna mwanafunzi anavyopata somo, inalenga kubadilisha namna anavyoshiriki katika mchakato mzima wa kujifunza.
Kwa Mwalimu Alexina, safari hiyo haipaswi kuishia katika kubuni teknolojia moja. Anaamini ubunifu unapaswa kuendelea ili watu wenye ulemavu wa macho waweze kufahamu teknolojia kwa undani zaidi.
“Ningependa waongeze ubunifu na kufanya sisi wasioona tuweze kuifahamu teknolojia kwa undani, tuweze kufanikiwa katika shughuli zetu za kazi na masomo kwa ujumla,” anasema.
Kauli hiyo inaweka changamoto mbele ya wabunifu, taasisi za elimu na wadau wa teknolojia,
kuhakikisha ubunifu hauishii kwenye maonesho, bali unamfikia mtu anayehitaji na kutatua changamoto yake.
Miaka 40 ya Costech inatoa fursa ya kutazama safari ya Tanzania katika sayansi, teknolojia na ubunifu, lakini pia kujiuliza swali muhimu, je, ubunifu unaotengenezwa nchini unafikaje kwa wananchi na kubadili maisha yao?
Kwa Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dkt. Amos Nungu, vijana na wabunifu wana nafasi kubwa katika kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Anawahimiza kutumia fursa, ushauri na msaada unaotolewa na taasisi mbalimbali ili kukuza bunifu zao na kuzifikisha katika hatua ya matumizi.
“Tunapokuwa na vijana wenye bunifu, tunapaswa kuwapa nafasi na kuwaunga mkono ili waweze kufikia malengo yao,” anasema.
Hapa ndipo simulizi ya Porto inapokutana na ajenda pana ya Costech.
Si suala la kuwa na mbunifu mwenye wazo pekee. Ni suala la kujenga mazingira ambayo yanamwezesha mbunifu kulipeleka wazo hilo kwa mlengwa, kulijaribu, kuliboresha na hatimaye kulifanya kuwa sehemu ya suluhisho.
Changamoto kubwa kwa wabunifu wengi si kupata wazo, bali kulifikisha wazo hilo katika hatua ambayo linaweza kutumika na watu wengi.
Shio anasema kampuni yake inalenga kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwamo taasisi, shule, Serikali, wizara na kampuni zinazofanya kazi katika sekta ya mawasiliano, ili teknolojia hiyo iwafikie wanafunzi wengi zaidi wenye mahitaji maalum.
Huo ndio mnyororo unaohitajika katika safari ya ubunifu, mbunifu, taasisi, shule, Serikali, sekta binafsi na mtumiaji wa mwisho.
Bila mnyororo huo, teknolojia inaweza kubaki kwenye maonesho, ikiwa mnyororo huo utaimarishwa, teknolojia inaweza kuingia darasani na kubadili maisha.
Mtoto asiyeona si mtoto asiyeweza
Simulizi hii inafikisha ujumbe mkubwa zaidi ya teknolojia yenyewe.
Mwanafunzi asiyeona hahitaji kuhurumiwa pekee, anahitaji mazingira yanayompa nafasi ya kuonyesha uwezo wake.
Anahitaji kitabu anachoweza kukifikia. Anahitaji mwalimu anayoweza kuwasiliana naye. Anahitaji teknolojia inayomruhusu kujifunza. Na zaidi, anahitaji kuamini kuwa ulemavu wake si mwisho wa ndoto zake.
Hapo ndipo thamani ya ubunifu inapopimwa.
Si kwa ukubwa wa mashine.
Si kwa idadi ya teknolojia zilizotengenezwa.
Bali kwa maisha ambayo teknolojia hiyo imeweza kubadilisha.
Kwa Mwalimu Alexina, teknolojia hiyo inaweza kuwa chachu ya kuwaongezea wanafunzi ufanisi katika masomo na kuwafungua zaidi katika ulimwengu wa teknolojia.
Kwa Shio, ni hatua ya kutumia ubunifu wa ndani kutengeneza suluhisho kwa changamoto inayowakabili Watanzania.
Na kwa Costech, ni sehemu ya simulizi ya miaka 40 inayopaswa kuendelea, kujenga mazingira ambayo sayansi, teknolojia na ubunifu haviishii kwenye karatasi, maabara au maonesho, bali vinafika kwenye jamii.
Miaka 40 ya Costech inaweza kuwa kumbukumbu ya safari iliyopita, lakini pia inaweza kuwa mwanzo wa sura mpya ya Tanzania inayotaka kutumia maarifa kutatua changamoto zake.
Ubunifu wa Porto unaonyesha kuwa baadhi ya majibu tunayoyatafuta yanaweza kuwa ndani ya nchi, yakitokana na mawazo ya vijana na wabunifu wanaoona changamoto na kuamua kuzigeuza kuwa fursa ya kutengeneza suluhisho.
Kwa mwanafunzi asiyeona, teknolojia hii inaweza kuwa zaidi ya kifaa.
Inaweza kuwa ufunguo wa kitabu, darasa na maarifa.
Na hapo ndipo maana halisi ya kuwekeza katika sayansi, teknolojia na ubunifu inapopatikana si katika idadi ya bunifu zilizotengenezwa, bali katika idadi ya maisha yanayobadilishwa na bunifu hizo.
Hiyo ndiyo Tanzania inayoweza kuingia katika miaka 40 ijayo ya Costech ikiwa na swali moja mbele yake, tunaweza kufanya nini zaidi kuhakikisha kila ubunifu una uwezo wa kumfikia Mtanzania anayehitaji suluhisho?

You Might Also Like

Matukio ya Wafanyakazi Yaliyojiri kuanzia Januari 2024, Hadi Leo Disemba 31, 2024

Inzi Chuma: Suluhisho la Chakula cha Mifugo, Uhifadhi wa Mazingira

Bima Ya Afya Kwa Wote: Safari Ya Kumfikia Kila Mwananchi

Rais CWT Ni Kiongozi Aliyekuza Taaluma Kwa Moyo, Sio Cheo

Sanaa, Utamaduni Yaimarisha Urafiki Wa China, Afrika

Share This Article
Facebook Twitter Whatsapp Whatsapp Email Copy Link Print
Previous Article Mkenda: Bunifu Zigeuke Bidhaa Na Biashara
Leave a comment Leave a comment

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Stay Connected

235.3kFollowersLike
69.1kFollowersFollow
11.6kFollowersPin
56.4kFollowersFollow
136kSubscribersSubscribe
4.4kFollowersFollow
- Advertisement -
Ad imageAd image

Latest News

Mkenda: Bunifu Zigeuke Bidhaa Na Biashara
Habari August 20, 2026
Barabara Zinazopasuka, Suluhisho Linalotoka Maabara za Tanzania
Makala August 19, 2026
Mnyama Check App: Ubunifu Wamtoa Mfugaji Gizani hadi Kidijitali
Makala August 18, 2026
Waziri Mkenda Kuzindua Wiki Ya Elimu,Ujuzi Na Ubunifu,Washiriki Takriban 300 Waonesha Bunifu Mbalimbali
Habari August 17, 2026
//

To be acknowledged as Africa’s premier and most reliable digital media network, delivering exceptional content across all our platforms by 2025.

Sign Up for Our Newsletter

Subscribe to our newsletter to get our newest articles instantly!

MFANYAKAZI TANZANIAMFANYAKAZI TANZANIA
Follow US
© 2024 Mfanyakazi Tanzania. All Rights Reserved.
Welcome Back!

Sign in to your account

Lost your password?