Na Lucy Ngowi
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu nchini ili bunifu zao zisitumike kama maonesho pekee, bali zigeuke kuwa bidhaa na biashara zitakazochangia uchumi wa Taifa.
Profesa Mkenda ameyasema hayo wakati akifungua rasmi Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026, katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, Agosti 18, 2026.
Amesema Serikali tayari imeshuhudia mafanikio kupitia mashindano ya ubunifu, ambapo baadhi ya bunifu zimeingia sokoni na kuwa chanzo cha kipato kwa wabunifu, zikiwamo mashine ya kukamua mafuta ya parachichi, mabegi ya shule yenye sola, vifaa vya kusaidia wanafunzi wenye ulemavu, teknolojia za usindikaji wa chakula cha mifugo na mita janja za maji.
Amesema Serikali inafuatilia takribani bunifu 70 katika hatua mbalimbali za maendeleo na inaendelea kushirikiana na taasisi na sekta binafsi kuzisaidia kufikia hatua ya kibiashara.
“Lengo ni kuhakikisha bunifu hazibaki kwenye maonesho pekee, bali zinakuwa bidhaa zinazotumika na kuleta matokeo kwa jamii na uchumi,” amesema.
Aidha, amesema hadi sasa halmashauri 90 zimeanzisha Madawati ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, huku Serikali ikiwa na mpango wa kuyafikisha katika halmashauri zote nchini. Serikali pia, kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, imeweka utaratibu wa kuwasaidia wabunifu kupata mitaji, huku ikiendelea kushirikiana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi kutafuta masoko, utaalamu na fursa za uwekezaji.
Katika hatua nyingine, Ofisa Uhusiano Mwandamizi kutoka Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR), Maryciana Mhagama, amesema Diplomasia ya Uchumi ya Serikali ya Tanzania inalenga kuimarisha nafasi ya nchi kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa, hususan maeneo huru ya biashara barani Afrika.
Mhagama ameyasema hayo katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Tanga, ambako CFR ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.
“Pamoja na mambo mengine, Uhusiano wa Kimataifa umeweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi, Uwekezaji, ukuaji wa Biashara, Mikutano, Utamaduni na Utalii. Kwa kuzingatia fursa zilizopo, Tanzania inaendeleza Diplomasia ya Uchumi katika Uhusiano wa Uwili, Kikanda na Kimataifa,” amesema Mhagama.
Akizungumzia mafunzo yanayotolewa na Kituo hicho, amesema kinaendelea kuwaandaa vijana wa Kitanzania kuwa mahiri na wenye weledi kitaaluma, wazalendo na raia wema wenye utayari wa kutoa mchango kwa Taifa.
Amesema Kituo kinatoa mafunzo na kozi mbalimbali katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia, Menejimenti ya Uhusiano wa Kimataifa, Utawala wa Kimkakati na Diplomasia ya Uchumi.
Mhagama amesema Kituo kimeandaa mafunzo kuhusu Diplomasia, Itifaki na Ustaarabu, “Diplomacy, Protocol and Etiquette”, yatakayofanyika kuanzia Agosti 24 hadi 28, 2026, CFR, Dar es Salaam, akiwataka wadau kutoka taasisi za umma na sekta binafsi kutumia fursa hiyo.
Wiki hiyo yenye kaulimbiu “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050” inaendelea hadi Agosti 24, 2026.

