Na Lucy Lyatuu
MBIO za Mkunga Marathon zinatarajiwa kufanyika Mei 2 mkoani Kilimanjaro zikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mkunga Duniani, huku zikilenga kukusanya fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za uzazi nchini.
Akizungumzia tukio hilo, Cedou Mandingo maarufu kama ‘Babu wa Kitaa’ ameishukuru Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) kwa kumteua kuwa balozi, akiahidi kuunganisha jamii na wakunga pamoja na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa taaluma hiyo.

“Nitahakikisha naunganisha Chama cha Wakunga na jamii, lakini pia kupeleka elimu ili watu waelewe mkunga ni nani na ana nafasi gani katika kuokoa maisha ya mama na mtoto,” amesema Mandingo.
Ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo kwa kujisajili mapema, akisisitiza kuwa ushiriki wao utasaidia kufanikisha lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Kwa mujibu wa Rais wa TAMA, Beatrice Mwilike, mbio hizo zinatarajiwa kushirikisha zaidi ya watu 2,000, zikiwa na vipengele vya kilomita 5, 10 na 21.
Amesema fedha zitakazokusanywa zitatumika kununua vifaa tiba muhimu kwa ajili ya kuboresha huduma za uzazi, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kushiriki kwa ada ya shilingi 35,000.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu nafasi ya wakunga katika kuhakikisha uzazi salama na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

