Na Danson Kaijage
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Dodoma Mjini kupitia CCM, Samwel Malecela, ameahidi atatoa kipaumbele kwa vijana kwa kuanzisha shule maalum ya kuibua vipaji kuanzia utotoni.
Akizungumza na wajumbe wa CCM katika Kata ya Mpunguzi, Malecela amesema vipaji vimekuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana duniani kote, hivyo kuvitambua na kuviendeleza mapema ni njia sahihi ya kuwawezesha kiuchumi.
Amesema shule hiyo itakuwa kichocheo cha kuongeza kipato kwa vijana na kuchangia pato la jimbo zima.
“Leo hii vipaji ni ajira, na iwapo watoto wetu wataandaliwa mapema, watakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa kuliko kusubiri hadi mtu awe mtu mzima,” amesema.
Sambamba na hilo, ameahidi kushughulikia upatikanaji wa mikopo ya halmashauri kwa wakati kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Amesema akiwa mbunge, atatumia nafasi yake kushinikiza utoaji wa mikopo hiyo usicheleweshwe, kwani ni haki yao kwa mujibu wa sera za serikali.
Aidha, Malecela alizungumzia mpango wa kuvutia wawekezaji hasa katika kata ya Matumbulu, ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa maeneo hayo.
Amesema pia changamoto ya maji kama moja ya kipaumbele atakachoshughulikia kwa kushirikiana na serikali kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Vile vile amesema Katika kata ya Mkonze, Samwel Malecela amekemea vikali vitendo vya upotevu wa mali za umma na migogoro ya ardhi vinavyoathiri maendeleo ya wananchi.
Akijibu maswali ya wajumbe wa CCM katika kata hiyo, amesema hatakubali wananchi kuendelea kunyimwa maendeleo kwa sababu ya ubadhirifu wa wachache.
“Baadhi ya watumishi wamekuwa wakihusika na ufisadi wa mali za umma huku wananchi wakibaki masikini.
“Hili ni jambo nitakalokomesha nikiwa mbunge,” amesema.
Pia aliahidi kushughulikia kero ya barabara kwa kuhakikisha zinajengwa kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika kwa urahisi.