Mwandishi Wetu
MWANZA: TAASISI ya Wanahabari ya Usaidizi kwa Jamii za Pembezoni (MAIPAC) kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) wamezindua mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari za mazingira wa Kanda ya Ziwa, yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kuandika kwa weledi pamoja na kuwasaidia kuelewa sheria mbalimbali zinazohusiana na mazingira.
Mafunzo hayo yanahusisha waandishi wa habari 35 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, na ni sehemu ya utekelezaji wa programu endelevu inayofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Kabla ya mafunzo hayo, awamu ya kwanza iliwahusisha waandishi wa habari kutoka Kanda ya Kaskazini.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Miradi wa THRDC, Wakili Halima Sonda, amewataka waandishi wa habari kuzingatia uandishi wa habari za kiuchunguzi zinazohusu mazingira ili kusaidia jamii kupata taarifa sahihi na kuchukua hatua dhidi ya changamoto za kimazingira.
Amesema jamii zimekuwa zikiathirika kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira, hivyo vyombo vya habari vina jukumu muhimu la kuelimisha umma na kusaidia kupunguza athari hizo kupitia taarifa za kitaaluma na zenye ushawishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma Siwayombe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), amewataka wanahabari kufahamu vyanzo vya uharibifu wa mazingira na mbinu za kukabiliana navyo.
Amesema uandishi wa habari za mazingira unahusisha maeneo mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, ukame, uhifadhi wa wanyamapori, kilimo pamoja na mipango bora ya matumizi ya ardhi.
Siwayombe amesisitiza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanahabari kuandika habari za kina na za kiuchunguzi zitakazosaidia kuibua changamoto za mazingira, kushawishi maboresho ya sera na sheria, na hatimaye kulinda jamii zinazoathirika.
“MAIPAC na THRDC tutaendelea kuwasaidia ili mtimize wajibu wenu. Tunataka kuona matokeo chanya kutoka kwenye mafunzo haya,” amesema.
Naye Wakili Paul Kisabo alipokuwa akitoa mada kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya mazingira, amewataka wanahabari kuzifahamu sheria hizo ili kuimarisha weledi katika kazi zao na kuepuka changamoto za kisheria.
Pia amewahakikishia wanahabari kuwa wataendelea kupata msaada wa kisheria pale wanapokumbana na changamoto za kikazi, hususan katika uandishi wa habari za kiuchunguzi na masuala ya maslahi ya umma.
Mwanahabari mkongwe, Edwin Soko, amewataka washiriki kutambua jukumu lao kubwa la kuwa sauti ya wasio na sauti katika jamii, hususan katika masuala yanayohusu ulinzi wa mazingira.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea katika kanda nyingine nchini, yakiwa na lengo la kuongeza wigo wa uelewa kwa wanahabari kuhusu uandishi wa habari za mazingira na sheria zake.


