Na Lucy Lyatuu
MCHUNGAJI Richard Hananja amewataka vijana kutafakari kwa kina kabla ya kushiriki maandamano au vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi, akisisitiza kuwa tofauti za mitazamo zinapaswa kujenga mazungumzo na maelewano, si migawanyiko.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 18, 2026, Hananja ameonya dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoweza kuchochea chuki, matusi na vurugu, huku akiwahimiza vijana kutumia majukwaa hayo kwa uwajibikaji.
Amesema vijana wanapaswa kuwa waangalifu na wito unaotolewa mtandaoni, akibainisha kuwa wengi wa wanaohamasisha maandamano na vurugu hawapo nchini na hawaathiriki moja kwa moja na madhara yake, huku athari kubwa zikiwakumba wananchi waliopo nchini.

