Na Lucy Lyatuu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi ) Mohamed Mchengerwa amewataka watendaji wa mradi wa mabasi yaendayo haraka ,Dar es Salaam (DART)
kutoa fursa kwa watanzania wenye uwezo kuwekeza katika mradi huo ili kupunguza changamoto na kero zinazolalamikiwa hasa msongsmano wa watu katika vituo kwa muda mrefu .
Aidha amewaagiza watendaji hao kutokaa maofisini na kwenda katika vituo hivyo kutatua changamoto za wananchi.
Mchengerwa ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa kadi janja na mageti ya mfumo wa kielektroniki ulioanza kutumika kuanzia leo katika vituo mbalimbali hapa jijini.
Uzinduzi huo umefanyika katika kituo kikuu Cha mabasi hayo Kimara Mwisho na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wananchi wa maeneo mbalimbali.
“Masuala ya kubishana bishana hatuyataki watanzania wanataka huduma ili kuepusha usumbufu mkubwa uliopo katika usafiri huu kila siku michakato isiyomalizika sitaki kuisikia na kuanzia Leo msikae maofini tokeni nendeni mkawahudumie Watanzania,”amesema Mchengerwa.
Amesema wapo watanzania wanaweza hivyo washirikishwe wawekeze kwani kama Mtanzania ana mabasi yanayokwenda Mwanza, Arusha na sehemu nyingine hawezi kushindwa kuhudumia mabasi kama haya na sio kuwaangalia wazabuni wa nje tu,.
Amewataka DART na UDART kuhakikisha mabasi yanakamilika katika maeneo yote yenye barabara hizo ikiwemo Mbagala kabla ya Desemba mwaka huu ili watanzania wafurahie matunda ya Serikali yao.
“Sisi tumeaminiwa kuhakikisha Watanzania wanapata huduma nzuri naamini mtatoa elimu zaidi kuhusu tandao wa Mwendokasi App ili Watanzania wawe na uelewa mpana katika ukataji tiketi ili kuepuka kero zilizokuwepo awali,” amesema.
Amesema anaimani huduma ikiwa nzuri hata watu wenye magari yao binafsi wanaweza kuegesha magari yao na kutumia usafiri huo wenye haraka zaidi.
Mchengerwa amewataka warendaji wote katika Wizara hiyo wabadilike na kuhakikisha wanafuata muda wa mabasi kufika vituoni ili kupunguza msongamano usiokuwa na tija kwa abiria.
Amewataka watendaji kusitisha mara moja matumizi ya tiketi za karatasi na kuanza kutumia kadi janja ambazo pia amewataka kuziweka katika mfumo rafiki ili kupunguza wingi wa kadi kwa wananchi.
Mchengerwa amesisitiza kuhakikisha wanatatua na kumaliza kero ili wakifika katika majiji mengine ikiwemo Arusha, Mwanza na Mbeya hapa Dar es Salaam kusiwe na changamoto yoyote ile.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa DART Othman Kihamia amesema mfumo huo utakuwa bora na kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwepo mfano chenchi, foleni kwa wananchi waliokiwa wakikutana nazo huko nyuma.
“Kadi hizo zina ubora wa hali ya juu na tumejipanga kuhakikisha watanzania hawakutani na changamoto kama zilizokuwepo huko nyuma,”alisema.