Na Mwandishi Wetu
MOROGORO: CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kimeendelea kukuza uelewa na umahiri wa vitendo kwa wanafunzi kwa kutumia ngamia katika mafunzo yanayowasaodia kuwa madaktari wenye weledi.
Wanafunzi wanaotumia ngamia katika mafunzo yao ni kutoka Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya.
Msimamizi wa Shamba la Utafiti katika ndaki hiyo, Enesa Mlay amesema hayo alipokuwa akitoa mafunzo ya namna ya kuwapa ngamia dawa za minyoo kwa njia ya sindano kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Stashahada ya Afya ya Wanyama na Uzalishaji wanaosoma chuoni hapo.
Amesema SUA inaendelea kuboresha ufugaji wa ngamia kwa ajili ya tafiti, elimu na mafunzo kwa wanafunzi wa taaluma mbalimbali lengo kubwa likiwa ni kuwawezesha wahitimu wa chuo hicho kufanya kazi zao kwa ufanisi na umahiri mkubwa.
“Ngamia wamekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wetu wanaosomea Tiba ya Mifugo, Sayansi ya Wanyama, Kozi za Ualimu na hata wale wanaosomea Misitu, ambapo hujifunza namna ya kuwatambua, kuwahudumia na kutambua tabia zao,” amesema.
Amesema mafunzo hayo huwasaidia wanafunzi hao kujiandaa kikamilifu kwa maisha ya kitaaluma pindi wanapomaliza masomo yao kwa kuwa katika shamba hilo la utafiti, wanafunzi hujifunza pia namna ya kushughulika na magonjwa ya ngamia ukiwemo ugonjwa wa kuharisha ambao ni hatari kwa mnyama huyo.
Akimwelezea mnyama huyo amesema, ngamia ni mnyama wa kipekee mwenye faida nyingi na anayeweza kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo kuwataka wafugaji kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na ufugaji wa ngamia.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma Shahada ya Afya ya Wanyama na Uzalishaji wamefurahishwa na mafunzo hayo kwa vitendo na kusema yanawajengea hali ya kujiamini kiasi kwamba watakapohitimu watakuwa madaktari wazoefu, hivyo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.