Na Danson Kaijage
DODOMA:TAASISI ya Tiba ya Mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu (MOI) kwa miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, imefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh. Bilioni 150 kwa ajili ya wangonjwa ambao wangetibiwa nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema hayo alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari katika ukumbi wa Habari Maelezo Jijini Dodoma,juu ya mafanikio ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassani.

Dkt.Ulisubisya amesema kwa kipindi cha miaka minne taasisi hiyo imeweza kutoa huduma bingwa za kimatibabu na kuweza kuokoa mabilioni ya fedha kwa wagonjwa ambao wametibiwa ndani ya nchi badala ya kutibiwa nje ya nchi.
Amesema huduma muhimu zinazotolewa na MOI ni pamoja na kutoa huduma ya mkono wa umeme ambapo mpaka sasa wagonjwa sita wamewekewa mkono bandia.
Vile vile kutengeneza viungo bandia kwa teknolojia ya ‘3D’ kwa wagonjwa wanne .

Pia amesema kuwa MOI imeanzisha huduma mpya za kibingwa na kibobezi ambazo hazipatikani hapa nchini kama vile benki ya mifupa, na matibabu ya ‘Parkinsons’ pamoja na kutetemeka.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne, Taasisi ya MOI imefanikiwa kutoa huduma za kibobezi kwa wagonjwa 7,366.
Amesema kuwa Gharama za matibabu hayo ndani ya nchi zilikuwa Sh. Bilioni 68 na kama wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu jumla ya Sh. Bilioni 218,zingetumika.
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa serikali imefanikiwa kuokoa Sh. Bilioni 150 ambazo zimetumika katika shughuli nyingine za maendeleo.
Akizungumzia mipango ya baadaye amesema Taasisi inaendelea kuboresha huduma kwa viwango vya kimataifa kwa Ujenzi wa hospitali ya kisasa ya utengamao katika kiwanja cha MOI chenye ukubwa wa hekari 10 kilichopo Mbweni Mpiji jijini Dar es salaam.
Pia kusogeza huduma katika jengo ambalo lilikua linatumika na Hospitali ya Tumaini upanga ili sehemu ya wagonjwa wa nje waanze kupata huduma katika jengo hilo na kupunguza msongamano MOI.