Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WATAFITI zaidi ya 100 kutoka mataifa 10 ulimwenguni wamekutana katika kongamano la Elimu lililoandaliwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuwasilisha na kujadili matokeo ya tafiti zao mbalimbali walizozifanya kuhusiana na elimu msingi na kutoa mapendekezo namna ya kuikuza elimu hiyo nchini.
Akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahera amesema mada zinazowakutanisha watafiti hao ni muhimu, zijadiliwe kwa kina kwani zinaendana na malengo ya sasa ya nchi,
Hivyo maarifa yatakayotolewa na mijadala yafikishwe wizarani ili kuona namna bora ya kuweza kuyatumia katika kuboresha juhudi zinazofanyika.
“Kuna mapitio makubwa katika sera na mitaala ya elimu nchini, ambapo elimu msingi inachukuliwa kama nguzo muhimu ya kuandaa watoto kuwa na uwezo wa kuwa na fikra tunduizi, mbunifu na maadili ya Kitanzania. Hivyo, kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, wataalam hawa watawasilisha machapisho yao na kuweza kujadili namna gani bora, elimu msingi inaweza kutekelezwa vizuri,” amesema.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Elifas Bisanda, amesema chuo hicho kimekuwa ni nguzo muhimu katika kuimarisha ubora wa elimu ya msingi nchini kwani kimekuwa kikitoa mafunzo ya stashahada ya elimu ya msingi tangu 2008 ili kukabiliana na upungufu wa walimu katika ngazi hiyo.
“Pia kongamano hili ni sehemu ya Maadhimisho ya 30 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, chuo hiki kimekuwa mbele katika kuendeleza na kuimarisha elimu ya msingi. Baada ya kuanzishwa shule za sekondari nyingi kwenye kata, walimu wenye stashahada walihamishwa kufundisha sekondari hivyo tulianzisha stashahada ya elimu ya msingi na hata walimu waliomaliza stashahada hiyo walibaki kufundisha shule hizo wakiwa na maarifa bora zaidi,” amesema.
Dkt. Janeth Kigobe, Mhadhiri Mwandamizi na Katibu wa kongamano hilo la kimataifa, amesema kumekuwa na haja ya kujadili elimu msingi na kuweka mikakati namna ya kushawishi serikali mbalimbali duniani hususani Tanzania namna ya kukuza elimu msingi kwa manufaa makubwa ya maendeleo ya nchi.
Kabla ya kongamano hilo, kulifanyika matembezi ya hisani katika kitongoji cha Kwamfipa mjini Kibaha ambayo yalilenga kuhamasisha umma kuhusiana na umuhimu wa elimu msingi nchini.
Kongamano hilo lenye ujumbe wa “Uboreshaji wa Elimu Msingi kwa Maendeleo Endelevu” linafanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani ambapo wanazuoni kutoka nchi za Uganda, Zambia, Jamaica, Uswisi, Uholanzi, Jamhuri ya Kongo, Nigeria, Kenya, na wenyeji Tanzania Bara na Zanzibar watakutana kwa pamoja kujadili mustakabali wa elimu msingi.