Korea Kusini yafungua fursa za utafiti, ubunifu, uhamishaji teknolojia na ajira kwa Watanzania
Na Mwandishi Wetu,
Incheon, Korea Kusini: TANZANIA iko mbioni kupata fursa mpya za utafiti, ubunifu, uhamishaji wa teknolojia na ajira za kisasa baada ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Kongani ya Ubunifu ya Incheon (IIC) kuweka msingi wa kuanzisha tawi la IIC nchini.
Ushirikiano huo unalenga kuwaunganisha watafiti, wabunifu na wataalamu wa Tanzania na mfumo wa ubunifu wa Korea Kusini, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa Watanzania kuendeleza teknolojia kutoka hatua ya utafiti hadi matumizi ya kibiashara.
Hatua hiyo imeainishwa Septemba 3, 2026, wakati wa hafla ya IIC Global Branch MOU Ceremony iliyofanyika Songdo Convensia, Incheon, Korea Kusini, sambamba na Mkutano wa Kimataifa wa Teknolojia za Mazingira wa Incheon 2026.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Noel Kaganda, amesema ushirikiano huo unapaswa kujenga uwezo wa pande zote badala ya Tanzania kubaki mtumiaji wa teknolojia zinazozalishwa na wengine.
“Ubunifu lazima uwe shirikishi. Hatupaswi kuwa na nchi moja inayozalisha na nyingine inayobaki kuwa mtumiaji pekee katika ikolojia ya ubunifu,” amesema.
Amesema Tanzania inapaswa kutumia fursa hiyo kujenga mazingira yatakayowawezesha wataalamu wake kushiriki katika kubuni, kuendeleza na kujaribu teknolojia zinazokidhi mahitaji ya nchi.

Makubaliano hayo yameainisha ushirikiano katika utafiti wa pamoja, maendeleo ya teknolojia na ubunifu, uhamishaji wa teknolojia, ubia wa kibiashara pamoja na shughuli za kitaaluma na kitaalamu.
Kwa vijana na wataalamu, ushirikiano huo unaweza kufungua nafasi za kupata ujuzi kupitia miradi ya pamoja na taasisi za utafiti, kampuni na wataalamu wa Korea Kusini, huku ukiongeza uwezekano wa bunifu za Kitanzania kufikia soko na kuanzisha biashara.
Aidha, makubaliano hayo yametoa nafasi ya kuandaa ramani ya kimkakati kuelekea kuanzishwa kwa Kituo cha Sayansi na Teknolojia cha K-Africa.
Balozi Kaganda amesema ushirikiano huo ni sehemu ya diplomasia ya sayansi, teknolojia na ubunifu na kuitaka COSTECH na IIC kuhakikisha makubaliano hayo yanazaa matokeo yenye tija.
Hatua hiyo imeendana na msisitizo wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, aliyehimiza Tanzania kujifunza uzoefu wa Korea Kusini katika kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kuchochea maendeleo ya uchumi.


