Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Author 6

Ujenzi Sports Club Yatoa Msaada Kwa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum, Dodoma

Na Mwandishi Wetu
TIMU  ya Ujenzi Sports Club imeendelea kuunga mkono juhudi za kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wa shule ya msingi Mlezi jijini Dodoma.
Msaada huo umetolewa  ikiwa ni sehemu ya juhudi za Ujenzi Sports Club kuunga mkono kazi inayofanywa na shule hiyo katika kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanafunzi wengine kupata mazingira bora ya kujifunzia.
Habari Picha 13581
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na madaftari, vyombo vya kulia chakula, vifaa vya usafi, sabuni, ndoo pamoja na fedha kwa ajili ya ununuzi wa mipira ya michezo.
Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Ujenzi Sports Club,  Ibrahim Chatila, amesema klabu hiyo inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na walimu katika kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kutimiza ndoto zao kielimu na katika maisha kwa ujumla.
Habari Picha 13582
Amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada za Ujenzi Sports Club kuunga mkono juhudi zinazofanywa na shule hiyo, huku akiahidi kuwa klabu itaendelea kushirikiana na kuwahamasisha wadau wengine, hususan katika sekta ya ujenzi, kujitokeza na kusaidia juhudi hizo.
“Tunatambua kazi kubwa inayofanywa na walimu katika kuwalea na kuwawezesha watoto hawa. Msaada huu ni sehemu ya mchango wetu katika kuunga mkono juhudi hizo, na tutaendelea kuwahamasisha wadau wengine kujitokeza na kusaidia,” amesema  Chatila.
Habari Picha 13583
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mlezi,  Magreth Kisanga, ameishukuru Ujenzi Sports Club kwa ukarimu na moyo wa kujitolea uliouonyesha kwa kuwasaidia wanafunzi hao.
Amesema msaada huo utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa baadhi ya vitendea kazi vinavyohitajika katika kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia na kuishi shuleni.
Kwa upande wake, mwalimu anayesimamia kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum, Hashim Msemo, amesema wanafunzi hao wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao na wameendelea kufanya vyema katika mitihani yao.
Habari Picha 13584
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kuunga mkono juhudi za shule hiyo ili kuongeza fursa na mazingira bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Shule ya Msingi Mlezi ni shule jumuishi inayotoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanafunzi wengine, kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya elimu na maendeleo.
Habari Picha 13585
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.