Na Lucy Lyatuu,Morogoro
TAASISI ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imewahimiza vijana na wadau wa sanaa nchini kutumia fursa za mafunzo inayotoa ili kukuza vipaji, kuongeza ujuzi na kujenga uwezo wa kujiajiri kupitia sekta ya sanaa na utamaduni.
Akizungumza katika Tamasha la Nne La Taifa La Utamaduni linaloendelea mkoani Morogoro, Naibu Mkuu wa TaSUBa, Gabriel Kiiza, amesema taasisi hiyo inatoa programu mbalimbali zinazolenga kuwajengea wanafunzi uwezo katika maeneo tofauti ya sanaa, ikiwemo sanaa za maisha na ufundi, uzalishaji wa filamu na uigizaji, pamoja na uzalishaji wa muziki na sauti.
Kiiza amesema programu hizo zinapatikana katika ngazi za mwaka mmoja kwa ajili ya kupata cheti na miaka miwili kwa ngazi ya diploma, huku TaSUBa pia ikitoa mafunzo ya muda mfupi ya mwezi mmoja hadi miwili kwa watu wanaotaka kuongeza ujuzi katika eneo fulani la sanaa.
Amesema mafunzo ya muda mfupi yanamruhusu mtu mwenye kiwango chochote cha elimu kuchagua eneo analotaka kujiongezea ujuzi, akisisitiza kuwa shughuli za sanaa zinaweza kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa mtu binafsi bila kuathiri shughuli nyingine anazofanya.
Amesema vipaji vinahitaji kuendelezwa kwa elimu kwamba mwenye kipaji cha sanaa anapaswa kupata maarifa na ujuzi unaoweza kumsaidia kukifikisha katika kiwango cha kitaalamu na kumwezesha kutumia kipaji hicho kiuchumi.
Ametoa wito kwa vijana na wadau wa sanaa nchini kuchangamkia fursa hizo, akieleza kuwa TaSUBa imekuwa ikizalisha wahitimu wanaofanya kazi katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi, huku wengine wakipata fursa ya kuendelea na elimu ya juu ndani na nje ya Tanzania.
Amesema kwa wanaotaka kujiunga na programu za muda mrefu, TaSUBa inaendelea kupokea maombi hadi Septemba 10, 2026.


