Na Lucy Ngowi
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimeendelea kutumia teknolojia za kisasa kubadili mfumo wa utoaji wa elimu, kuwawezesha wanafunzi kusoma wakiwa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi bila kulazimika kufika chuoni.
Hatua hiyo imeifanya elimu ya masafa kuwa sehemu muhimu ya utoaji wa elimu katika chuo hicho, huku wanafunzi wakitumia majukwaa ya kidijitali kujifunza, kuwasiliana na walimu na kufanya mitihani kulingana na mifumo inayotumiwa na chuo.

Akizungumza katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi wa OUT, Dkt. Zacharia Rwejuna, amesema chuo hicho kimeendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa elimu kwa kutumia teknolojia za mtandao.
Amesema OUT inatoa programu kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamivu (PhD), zinazofundishwa kwa njia ya masafa na mtandao, hivyo kuwawezesha wanafunzi kuendelea na majukumu yao huku wakisoma.
“Katika maonyesho haya tumeleta programu zetu zinazotolewa kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamivu (PhD). Programu hizi zinafundishwa kwa njia ya masafa na mtandao, hivyo aina hii ya usomaji inaleta chachu ya ubunifu katika elimu,” amesema.
Dkt. Rwejuna amesema hapo awali wanafunzi walitegemea zaidi matini za kujisomea kabla ya kufika katika vituo vya mikoa kufanya mitihani, lakini mfumo huo umeendelea kuboreshwa kupitia matumizi ya majukwaa ya kidijitali, yakiwemo Moodle na Zoom.

Amesema majukwaa hayo yanawawezesha wanafunzi kuwasiliana na walimu na kushiriki vipindi vya masomo kwa njia ya mtandao, hatua inayopanua fursa za elimu kwa Watanzania na wadau waliopo nje ya nchi.
“Ubunifu tulio nao unalenga kuongeza ujuzi na tija katika ufundishaji, pamoja na kuwafikia wananchi wengi katika maeneo mbalimbali. Ubunifu huo unaonekana katika namna tunavyofundisha, tunavyofanya mitihani na hata katika mchakato wa usahihishaji,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ubunifu wa OUT, Dkt. Straton Ruhinda, amesema chuo hicho kinaendelea kuboresha mitaala yake ili kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaozingatia vitendo na mahitaji ya soko la ajira.

Amesema mfumo huo unawafaa watu wenye majukumu mbalimbali, kwa kuwa mwanafunzi anaweza kusoma akiwa mahali popote kwa kutumia kompyuta au simu janja, mradi awe na huduma ya mtandao.
Dkt. Ruhinda amesema kupitia mfumo wa ODEX, wanafunzi wanapata fursa ya kufanya mitihani kwa wakati unaowafaa kulingana na majukumu yao.
Amewahimiza wananchi kutumia fursa zinazotolewa na OUT kupata elimu, akisema matumizi ya teknolojia za kisasa yanaendelea kurahisisha upatikanaji wa elimu na kuwawezesha wanafunzi kufikia malengo yao.


