Mtumiaji wa bidhaa hizo asema matumizi ya dawa zinazotokana na magome ya korosho yanasaidia kupunguza utegemezi wa baadhi ya kemikali katika uchakataji wa ngozi
Na Lucy Ngowi
WAKATI mwingine uwekezaji katika sayansi na ubunifu huanza kwa kiasi kidogo, lakini matokeo yake yanaweza kuwa makubwa kuliko thamani ya fedha iliyowekezwa mwanzoni.
Hivyo ndivyo simulizi ya Dkt. Cecilia China, msomi kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), inavyoweza kueleweka.
Mwaka 2019, Dkt. Cecilia alikuwa miongoni mwa vijana walioshinda Mashindano ya Ubunifu ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) na kupata ufadhili wa Sh. Milioni 20 kutoka Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Miaka kadhaa baadaye, uwekezaji huo wa hatua ya mwanzo umeingia katika hatua ya biashara, uzalishaji na matarajio ya ajira kwa maelfu ya Watanzania.
Leo hii, Dkt. Cecilia ni mama wa watoto wawili, msomi, mjasiriamali na mmiliki wa kampuni pamoja na kiwanda jijini Arusha.

Lakini kinachofanya ubunifu wake uwe na umuhimu mkubwa zaidi ni kwamba hauishii kwenye bidhaa moja. Unaingia moja kwa moja kwenye mnyororo wa thamani wa korosho na mifugo, sekta mbili zenye uzito mkubwa katika uchumi wa Tanzania.
Maganda ya korosho: Taka au malighafi ya viwanda?
Tanzania ilizalisha zaidi ya tani 528,000 za korosho katika msimu wa 2024/25. Kwa kuwa ganda linachangia takribani asilimia 70 ya uzito wa korosho mbichi, kiasi cha maganda kinachoweza kuzalishwa endapo korosho hizo zitachakatwa kinaweza kufikia karibu tani 370,000.
Hii si kusema tani zote hizo sasa zinapotea Tanzania, bali ni kuonyesha ukubwa wa rasilimali ambayo inaweza kuingia kwenye uchumi wa mzunguko badala ya kuchukuliwa kama mabaki ya uzalishaji.
Na hapa ndipo ubunifu wa Dkt. Cecilia unapopata maana kubwa.
Maganda ya korosho yana kimiminika (Cashew Nut Shell Liquid – CNSL), kemikali yenye matumizi ya viwandani.
Makadirio ya kiteknolojia yanaonyesha kuwa CNSL inaweza kuwa takribani kilo 0.2 kwa kila kilo moja ya korosho mbichi. Kwa uzalishaji wa msimu wa 2024/25, hiyo inaonyesha uwezekano wa zaidi ya tani 105,000 za CNSL endapo malighafi yote ingechakatwa kwa kiwango hicho.
Kwa hiyo, ganda ambalo leo linaweza kuonekana kama taka linaweza kuwa malighafi ya kemikali, bidhaa ya viwandani na chanzo cha mapato kwa mkulima.
Kwa Dkt. Cecilia, hii ndiyo fursa anayolenga kuitumia katika uzalishaji wa dawa inayotumika katika usindikaji wa ngozi.
Mkulima wa korosho na mfugaji wanaingia kwenye mnyororo wa thamani moja
Kwa upande mmoja kuna mkulima wa Mtwara, Lindi, Pwani na maeneo mengine yanayozalisha korosho.
Kwa kawaida, thamani yake kubwa iko kwenye korosho yenyewe. Lakini kama maganda yanaweza kukusanywa na kuuzwa kama malighafi ya viwandani, mkulima anaweza kuanza kuona thamani katika sehemu ambayo awali haikuwa na thamani kubwa ya kibiashara.

Kwa upande mwingine kuna mfugaji.
Tanzania ilikuwa na takribani ng’ombe milioni 39.2 mwaka 2024, pamoja na mamilioni ya mbuzi na kondoo. Uzalishaji wa ngozi za wanyama ulifikia tani 55,410 mwaka huo.
Hii maana yake ni kwamba Tanzania ina malighafi kubwa ya kuendeleza sekta ya ngozi. Tatizo ni kwamba thamani kubwa bado haijakaa ndani ya nchi. Tunauza malighafi, wengine wanauza bidhaa yenye thamani.
Benki ya Tanzania iliripoti kuwa thamani ya ngozi ghafi iliyoingia sokoni ilifikia Sh. Bilioni 7.1 mwaka 2023/24, huku ngozi za ng’ombe zikichangia asilimia 82.6 ya thamani hiyo.
Lakini changamoto kubwa ni thamani ambayo Tanzania ilipoteza kwa sababu ya kuuza malighafi badala ya kusindika. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kinaonyesha Tanzania husindika takribani asilimia tano hadi 10 ya futi za mraba milioni 90 za ngozi ghafi inayozalishwa.
Tafsiri sahihi ni kwamba ng’ombe yupo Tanzania. Ngozi ipo Tanzania. Soko lipo. Lakini sehemu kubwa ya thamani ya mwisho hupotea, au hupelekwa nje ya nchi.
Ndiyo maana ubunifu wa Dkt. Cecilia wa kutengeneza dawa zinazotumika katika usindikaji wa ngozi unaweza kuwa muhimu kwa uchumi wa Tanzania.
Unaweza kuangalia ubunifu huu kama sehemu ya kujenga ikolojia ya viwanda vya ngozi Tanzania.Mtumiaji athibitisha umuhimu wa bidhaa, Uhitaji wa bidhaa zinazotumika katika uchakataji wa ngozi unaonekana pia kwa watumiaji wake.
Amir Mshana wa Usangi Leather Technology, wilayani Mwanga, Kilimanjaro, anasema ni mtumiaji wa bidhaa hizo na kwamba bidhaa zinazotumika katika uchakataji wa ngozi zina umuhimu mkubwa kiafya, hasa pale zinapotengenezwa kwa kutumia malighafi zisizoathiri afya ya binadamu.
Anasema wamekuwa wakitumia bidhaa za dawa zinazotokana na magome ya miti, ikiwamo magome ya korosho, katika uchakataji wa ngozi, badala ya kutegemea kemikali ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa afya.
Anasema bidhaa hizo zinatumika katika mchakato wa uchakataji wa ngozi na zimekuwa na manufaa kwao kutokana na kupunguza matumizi ya kemikali zinazoweza kuathiri afya ya binadamu.
Anasema jambo muhimu katika uchakataji wa ngozi ni kuhakikisha bidhaa zinazotumika ni salama kwa afya, kwa kuwa baadhi ya kemikali zinaweza kuleta madhara kwa binadamu.
Kiwanda kimoja kinaweza kuanzisha viwanda vingine
Kama dawa za usindikaji wa ngozi zinazohitajika na wasindikaji zinaweza kuzalishwa nchini kwa kutumia malighafi inayotokana na maganda ya korosho, kuna uwezekano wa kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Lakini faida inaweza kwenda mbali zaidi. Upatikanaji wa vitendea kazi vya ndani unaweza kusaidia kupunguza gharama za kusindika, kuchochea uwekezaji katika usindikaji, kuongeza uzalishaji wa ngozi laini na hatimaye kuchochea viwanda vya viatu, mikoba, mikanda na bidhaa nyingine za ngozi.

Hapo ndipo ajira zinapoanza kuongezeka kwenye mnyororo mzima, si kwenye kiwanda kimoja tu. Kuna ajira za kukusanya maganda ya korosho, kuna usafirishaji, na kuna kazi katika kiwanda cha kuzalisha dawa. Kuna watu watapata ajira za usindikaji ngozi, kuna viwanda vya bidhaa za ngozi na masoko na usambazaji ndani na nje ya nchi.
Na kuna fursa kwa wanawake na vijana kuingia katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani. Takwimu kutoka Afrika Magharibi zinaonyesha kuwa ajira 80 huzalishwa kwa kila tani 1,000 za korosho zinaposindikwa.
Kwa hiyo, uwezo wa ajira wa viwanda vya korosho unaweza kuwa mkubwa sana kadiri usindikaji unavyopanuka. Hizi si takwimu za ajira ambazo tayari zimezalishwa na Dkt. Cecilia, bali ni kiashiria kinachoweza kusaidia Serikali na wawekezaji kuona fursa kwa upana wake.
Kwa nini hilo ni jambo kubwa kwenye maadhimisho ya miaka 40 ya Serikali kuanzisha COSTECH?
Kuna sababu moja muhimu.
Sh. Milioni 20 za mwaka 2019 zilikuwa mbegu ya uwekezaji wa Serikali kupitia COSTECH iliyolelewa na taasisi mahiri ya NM-AIST.
Ikiwa ubunifu ulioanzishwa kwa fedha za Serikali utaimarishwa sokoni na kufanya uzalishaji mkubwa, kuunganisha wakulima wa korosho na wafugaji, kuchochea viwanda vya ngozi, kupunguza uagizaji wa kemikali, kuongeza mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani na kuunda ajira, basi faida yake ni ufunguo wa uchumi wa Mtanzania.
Hii ndiyo aina ya matokeo ambayo yanapaswa kuonekana wakati tunapozungumzia uwekezaji wa Serikali katika vijana, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Si kila ubunifu utakuwa kampuni kubwa. Si kila milioni 20 itazaa kiwanda. Lakini pale ambapo ubunifu unapofikia hatua ya kuunganisha malighafi ya kilimo, kemikali, kiwanda, ongezeko la thamani, ajira, hadi kukamata soko la dunia, ndipo tunaona kwa nini Serikali inapaswa kuwekeza katika hatua za mwanzo za ubunifu.

Mtwara inaweza kuwa zaidi ya kituo cha korosho
Mpango wa Dkt. Cecilia wa kuanzisha kiwanda kikubwa Mtwara unaweza kuwa na maana ya kimkakati. Mtwara ni kitovu cha uzalishaji wa korosho.
Hivyo, badala ya kusafirisha malighafi mbali ili kupata thamani, mfumo unaweza kujengwa ambapo sehemu kubwa ya mnyororo wa thamani inakaa karibu na chanzo cha malighafi. Mkulima anauza korosho. Kiwanda kinachakata korosho. Maganda yanakusanywa.
Maganda yanakuwa malighafi ya kemikali. Kemikali inatumika katika usindikaji wa ngozi. Ngozi ya mifugo inabadilishwa kuwa ngozi laini ya matumizi ya viwandani. Viwanda vinazalisha viatu, mikoba, mikanda na bidhaa nyingine. Bidhaa hizo zinauzwa ndani na nje ya Tanzania.Hapo ndipo taka inavyogeuka kuwa malighafi, malighafi kuwa kiwanda, kiwanda kuwa ajira, na ajira kuwa kipato.
Hii ndiyo Tanzania ya Dira 2050
Tanzania haiwezi kufikia uchumi mkubwa kwa kuuza malighafi pekee. Inahitaji kuongeza thamani ya kile ambacho tayari tunacho.
Tuna korosho.Tuna mifugo.
Tuna vijana.Tuna vyuo na watafiti.Tuna malighafi za viwandani. Tunachohitaji zaidi ni uwezo wa kuunganisha vitu hivyo kuwa bidhaa zenye thamani.
Ndiyo maana ubunifu wa Dkt. Cecilia China ni muhimu.
Ni mfano wa jinsi uwekezaji wa awali katika ubunifu unaweza kugeuka kuwa uwekezaji katika uchumi wa viwanda.
Na kama kiwanda chake kitafanikiwa kufikia uzalishaji mkubwa, maisha yake hayatakuwa tena kuhusu mwanamke mmoja aliyeshinda MAKISATU mwaka 2019.Habari kubwa itakuwa jinsi Sh. Milioni 20 zilivyoanza safari ya kujenga mnyororo mpya wa thamani unaowaunganisha wakulima wa korosho, wafugaji, wanawake, vijana, viwanda na masoko ya kimataifa.

Hii ndiyo sababu ubunifu wa Dkt. Cecilia China unapaswa kuangaliwa si kama bidhaa moja ya viwandani, bali kama mfano wa namna uwekezaji mdogo katika sayansi na teknolojia unavyoweza kujenga uchumi wa kesho.


