Na Lucy Lyatuu,Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete, ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuja na mfumo wa Kupanga na Kusimamia miradi ya Wakala huo.

Kikwete ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la Wakala huo,lililopo katika wiki ya Utumishi wa Umma 2026 inayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, mkoani humo.
Katika Mfumo huo (*REA DIGITAL PLATFORM*) unaonyesha miradi yote inayotekelezwa na REA na kuweza kuisimamia kidijitali na kuwapa taarifa wadau popote walipo duniani kuhusiana na miradi ya Nishati vijijini.

Akitoa maelezo yake kwa Waziri Kikwete, Ofisa Upimaji Mwandamizi wa REA, Hussein Shamdas ameeleza kuwa kupitia mfumo huo mwananchi anaweza kujua mipango ya Wakala kwenye eneo lake na kufuatilia miradi inayotekelezwa na Wakala katika eneo husika.


