Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa mchango wake katika kuimarisha afya ya mimea na kuongeza tija ya kilimo, akisema juhudi hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kuhakikisha usalama wa chakula na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo leo, Agosti mosi, mwaka huu 2026 alipotembelea banda la TPHPA wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya 33 ya Wakulima (Nanenane) 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru, ambaye amemweleza kuwa mamlaka hiyo imeongeza juhudi za kudhibiti visumbufu na magonjwa ya mimea, kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya viuatilifu na kuimarisha huduma za afya ya mimea ili kuongeza uzalishaji na kipato cha wakulima.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Nchemba amesema utendaji wa TPHPA unaakisi utekelezaji wa kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane mwaka huu 2026 isemayo, “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
Ameitaka mamlaka hiyo kuendelea kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa huduma za kitaalamu, ili kulinda mazao dhidi ya magonjwa na wadudu waharibifu, kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuimarisha usalama wa chakula nchini.







