Na Lucy Ngowi
MWANZA: MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu afya ya mimea pamoja na matumizi sahihi na salama ya viuatilifu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda afya ya binadamu, mazingira na viumbe rafiki.
Akizungumza katika Maonesho ya Ziwa Victoria yanayoendelea jijini Mwanza, Ofisa Kilimo wa mamlaka hiyo, Bakari Makomola, amesema matumizi ya viuatilifu yanapaswa kufanyika kwa kuzingatia kanuni na maelekezo sahihi ili kuhakikisha usalama wa mlaji, mtumiaji na mazingira kwa ujumla.
Amesema TPHPA iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Afya ya Mimea ya mwaka 2020 ina jukumu la kusimamia afya ya mimea pamoja na kudhibiti biashara ya viuatilifu nchini.
“Tunafanya usimamizi wa biashara ya viuatilifu, ukaguzi wa bidhaa hizo pamoja na kutoa leseni kwa waagizaji na wasambazaji,” amesema Makomola.
Ameongeza kuwa matumizi salama ya viuatilifu yanamaanisha kuhakikisha bidhaa hizo zinatumika kwa njia sahihi ili kulinda afya ya mlaji, mtumiaji na mazingira.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa wakulima na wadau wa kilimo ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi holela ya viuatilifu.

