Na Lucy Ngowi
MTAFITI Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) jijini Mwanza, Philemon Nsinda, amesema kuwa kutokana na upungufu wa samaki unaoendelea kujitokeza katika siku za karibuni, taasisi hiyo imefanya tafiti za kubaini maeneo yanayofaa kwa ajili ya ufugaji wa samaki katika Ziwa Victoria.
Nsinda amesema hayo alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa habari kwenye Maonesho ya Ziwa Victoria yanayoendelea jijini Mwanza.
Amesema maeneo yaliyobainishwa yamewasilishwa serikalini ili yaweze kutengwa na kugawiwa kwa wafugaji wa samaki wenye mahitaji ya kuendesha shughuli hizo.
“Katika siku za karibuni kumekuwa na upungufu wa samaki, hali ambayo imeongeza umuhimu wa kufuga samaki kwenye vizimba.
“Awali watu walifuga kwenye mabwawa, lakini sasa tunawashauri wafuge kwenye vizimba kwa sababu mavuno yake ni makubwa zaidi,” amesema Nsinda.
Aidha, ameeleza kuwa TAFIRI imekuwa ikiendesha tafiti mbalimbali zinazohusiana na uvuvi ili kubaini idadi ya samaki waliopo ziwani kwa kutumia mbinu za kisasa za kitaalamu, ikiwemo teknolojia ya mwangwi, inayosaidia kutoa makadirio ya samaki waliopo ndani ya ziwa.
Pia taasisi hiyo hufanya tafiti za kubaini kiwango cha samaki wanaovuliwa kutoka ziwani ili kupata takwimu sahihi za uzalishaji wa samaki.
Kwa upande wa baiolojia na mazingira, Nsinda amesema watafiti huangalia hali ya maji pamoja na kiwango cha uchafuzi wa mazingira kwa kuchunguza viashiria mbalimbali vinavyopatikana majini.
“Samaki wanahitaji mazingira mazuri ili waweze kuishi na kuzaliana vizuri. Maji yanapochafuka, uzalishaji wa samaki hupungua kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Vilevile, amesema taasisi hiyo hufanya tafiti za sayansi jamii zinazolenga kuwafahamu watu wanaotumia samaki kama sehemu ya lishe yao pamoja na wale wanaotaka kujihusisha na shughuli za uvuvi.
Ameongeza kuwa tafiti hizo husaidia kubaini mahitaji ya jamii na kutoa mwongozo sahihi kuhusu maendeleo ya sekta ya uvuvi nchini.
Nsinda amesema Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ina vituo vikubwa vinne vya utafiti, vikiwemo vya Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria pamoja na kituo cha baharini cha Kunduchi kilichopo Dar es Salaam.

