Na Lucy Lyatuu Dodoma
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeandika historia mpya katika sekta ya uhifadhi na utalii ikolojia baada ya kuongeza idadi ya watalii wa misitu hadi 329,753 na kukusanya zaidi ya Sh bilioni 3.09 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, hatua inayotafsiriwa kama mafanikio makubwa ya serikali katika kuigeuza misitu kuwa injini mpya ya uchumi wa utalii nchini.
Takwimu hizo zimetolewa bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara Ya Maliasili Na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema ongezeko hilo la watalii ni sawa na asilimia 20 ikilinganishwa na watalii 275,723 waliotembelea vivutio vya utalii ikolojia katika kipindi kama hicho mwaka uliopita, huku mapato yakiongezeka kwa asilimia 43 kutoka Sh bilioni 2.16 hadi kufikia Sh bilioni 3.09.
Amesema mafanikio hayo yanatajwa kuchochewa na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya utalii wa misitu, kampeni za matangazo na matukio ya michezo ya utalii yaliyoendelea kuvuta maelfu ya wageni wa ndani na nje ya nchi.

Katika mwaka uliopita pekee, TFS ilijenga malango sita ya kisasa katika maeneo ya Meru, Vikindu, Mwambesi, Pindiro, Mlima Rungwe na Ziwa Duluti; kujenga njia maalumu za watembea kwa miguu (board walks) katika misitu ya Sahare-Tanga na Amani; pamoja na kukarabati zaidi ya kilomita 287 za njia za watalii katika hifadhi 24 za misitu nchini.
“Mashindano na matamasha ya utalii yaliyofanyika ndani ya misitu yameendelea kuwa nyenzo mpya ya kutangaza vivutio vya Tanzania. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na Tukutane Mt. Rungwe Season II, Meru Adventure Race, Mkwawa Rally, Rombo Marathon, Kalambo Waterfalls Utalii Festival na Uni Pugu Easter Experience,” amesema.
Amesema i na mafanikio ya utalii, serikali imeendelea kuonyesha makucha katika vita dhidi ya uharibifu wa misitu na biashara haramu ya mazao ya misitu.

Waziri Kijaji amesema TFS ilifanya doria za kimkakati 363 na doria za kawaida 12,854 katika hifadhi mbalimbali, hatua iliyosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa 1,925 wa uhalifu wa misitu.
Amesema Kupitia operesheni hizo, serikali ilikamata na kutaifisha magunia 39,900 ya mkaa, mbao 31,046 zenye ujazo wa mita za ujazo 1,321, magogo 1,556 pamoja na mifugo zaidi ya 29,000 iliyokuwa ikiingizwa kwenye maeneo ya hifadhi kinyume cha sheria.
Katika hatua nyingine, TFS imeendelea kuimarisha vita dhidi ya moto wa misitu kwa kutumia teknolojia ya satelaiti kubaini matukio mapema, pamoja na kutoa mafunzo kwa vikosi 45 vya zimamoto na wananchi zaidi ya 20,000 wanaoishi jirani na hifadhi.
“Kutokana na juhudi hizo, matukio ya moto wa misitu yamepungua kwa wastani wa asilimia 11 kila mwaka, huku ukubwa wa maeneo yanayoteketea ukiendelea kupungua,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye upandaji miti na urejeshaji wa mazingira yaliyoharibiwa. Katika mwaka huu, TFS imeanzisha mashamba mapya ya miti ya Geita na Rwamgasa yenye ukubwa wa hekta 28,000, sambamba na kuzalisha miche milioni 32.8 ya miti iliyogawiwa kwa wananchi na taasisi mbalimbali kwa ajili ya upandaji.
Kuhusu mikoko, amesema zaidi ya miche milioni 37.2 imepandwa katika mikoa ya Tanga na Pwani kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, hatua inayolenga kuimarisha uhifadhi wa mwambao wa Bahari ya Hindi dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Sekta ya nyuki nayo imeendelea kuonyesha matumaini makubwa kiuchumi baada ya Tanzania kufanikiwa kuuza tani 1,076.8 za asali zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 12.9 katika masoko ya Ulaya na Marekani.
Waziri Kijaji amesema mafanikio hayo yamekuja baada ya sampuli 132 za asali kutoka wilaya 31 kupimwa katika maabara ya kimataifa nchini Ujerumani na kuthibitishwa kukidhi viwango vya ubora wa kimataifa.
“Matokeo yanaonyesha asali ya Tanzania ni bora na inakidhi vigezo vya kuuzwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema.


