Na Lucy Lyatuu,Dodoma
SERIKALI imepanga mikakati mbalimbali ya kukuza utalii kupitia matukio ya kimataifa yanayotarajiwa kufanyika nchini jambo litakaloongeza idadi ya watalii ,ajira na pato la taifa.
Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Ashatu Kijaji amesema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa Bunge jijini Dodoma na kuongeza kuwa sekta ya Utalii ni ya kimkakati na ya kimageuzi katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini .
Amesema , ili kufikia malengo hayo, Wizara inaendelea kutumia fursa na mikakati mbalimbali ya kukuza utalii kupitia matukio ya kimataifa yatakayofanyika nchini ikiwemo Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (Inter-Parliamentary Union – IPU Assembly), Mkutano huu unakutanisha Mabunge ya Nchi wanachama wa umoja wa mabunge Duniani na utafanyika tarehe 5 hadi 9 Oktoba, 2026 Jijini Arusha.

Amesema mkutano huo unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 1,500 wakiwemo Maspika 183 kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo Tanzania ni mwanachama na mwenyekiti wa umoja huo.
“Katika kuhakikisha Tanzania inafaidika kikamilifu na mkutano huu Wizara imeandaa na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutangaza mazao ya utalii na ukarimu,” amesema.
Vilevile, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa utalii itaandaa vifurushi vya tovuti ya IPU ambayo vitakuwa na link ambayo wageni wataweza kufanya booking ya kutembelea maeneo yetu moja kwa moja.
Amesema Pamoja na hilo, Wizara itaweka mabanda ya taarifa za utalii katika eneo la mkutano ili kuhamasisha washiriki kutembelea vivutio vyetu kipindi na baada ya mkutano kuisha. Pia, tovuti ya IPU itatumika kuweka taarifa za utalii na matukio mbalimbali ya wageni hao walipokua Tanzania ili kuendelea kuvutia wageni wengi zaidi kutembelea Tanzania.

iAmesema eneo lingine ni katika Tukio la World Travel A wards (WTA) 2026 ambalo ni la kimataifa huandaliwa kila mwaka kwa lengo la kutoa tuzo za ubora katika Sekta ya Utalii duniani.
Amesema , linatarajiwa kufanyika nchini Desemba, 2026 na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 1,000 kutoka Mabara ya Afrika, Ulaya, Asia, Amerika ya Kaskazini na Kusini.
“Wizara kwa kushirikiana na wadau wa utalii itaandaa vifurushi maalum vya mazao ya utalii na huduma kwa washiriki katika tovuti ya Bodi ya Utalii Tanzania na WTA pindi itakapofunguliwa,” amesema na kuongeza kuwa Wizara itatumia fursa za kidijitali, machapisho na taarifa mitandaoni kuwafikishia wadau mbalimbali taarifa muhimu za vivutio vya utalii Tanzania wakati wa tukio hilo.
Pia, Wizara itaendelea kuhamasisha wageni kutembelea vivutio vya utalii na maeneo mbalimbali kupitia vifurushi vilivyoandaliwa na kuwekwa katika jukwaa la utalii la TTB “booking platform”ili kuendelea kutoa wigo mpana kwa wageni kufanya uchaguzi wa kutembelea vivutio hata baada ya tukio hilo.
Amesema eneo lingine ni Shindano la 74 la UIimbwende wa Dunia 2027 – Miss World 2027
linalohusisha masuala ya urembo likiwa ni miongoni mwa mashindano makubwa duniani yanayojulikana kama Big Four Beauty Pageants.
Tukio hilo linatarajiwa kufanyika nchini Mei, 2027 na linatarajiwa kuhudhuriwa na watu takriban 20,000 wakiwemo washindani 120 kutoka nchi mbalimbali Duniani.
Aidha, kabla ya tukio hili, Wizara itawatangazia wadau na kuwahamasisha kuandaa na kuuza vifurushi vya safari kupitia jukwaa la utalii la TTB “booking platforms” na kutangaza tukio hili kupitia tovuti ya TTB, mitandao ya kijamii, televisheni, redio na vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi.
“Pamoja na hilo, Wizara itaandaa ziara ya mafunzo kwa kuwapa fursa Walimbwende na waandishi wa habari kutembelea maeneo ya vivutio (FAM Trip) kabla ya shindano kwa lengo la kukuza uelewa wa vivutio vyetu na kurusha maudhui hayo kwenye mitandao yao ya kijamii pamoja na kuvitangaza katika vyombo vya habari mbalimbali ulimwenguni,”amesema.

Kwa upande mwingine, Wizara itaweka mabanda ya kutangaza utalii na kutoa taarifa kwa watalii ndani ya maeneo yatakapofanyika mashindano na kuendelea kutumia maudhui ya mashindano hayo ikiwemo yatakayomhusu Mshindi wa Mashindano (Miss World) ili kujitangaza zaidi duniani.
Amesema baada ya shindano, Wizara kwa kushirikiana na wadau itaratibu safari za kutembelea vivutio kwa washiriki watakaokuwa wamejisajili kupitia jukwaa la utalii la TTB na washindi wa juu watano wa shindano hilo, watapewa ubalozi wa hiari wa kutangaza utalii wa Tanzania.
Dkt Kijaji amesema eneo lingine ni katika Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Nchi za Afrika (Africa Cup of Nations – AFCON) 2027
Amesema Mashindano hayo yanaandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kila baada ya miaka miwili (2) na kuhusisha timu za Mataifa kutoka Bara la Afrika.
Hata hivyo amesema Kwa mwaka 2027, mashindano hayo yanatarajiwa kuandaliwa kwa pamoja na nchi tatu za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania. Katika mashindano hayo, timu 24 zilizofuzu zitashindana na kutarajiwa kuwa na watazamaji wa viwanjani milioni 1.8 na wafuatiliaji katika televisheni bilioni 1.9 kupitia vituo vya utangazaji zaidi ya 185.
Aidha, mashindano hayo yanakadiriwa kuwa na faida za kiuchumi zinazoweza kufikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni mbili.
Amesema Kwa kuwa Tanzania ni moja ya waandaaji wa mashindano hayo, Wizara imeandaa mkakati wa kuitangaza Tanzania kama kivutio cha kipekee cha utali.
Amesema Mkakati huo unahusisha shughuli za kabla, wakati na baada ya mashindano ambapo kabla ya mashindano hayo, shughuli zinazotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na kuanza kutangaza utalii wa Tanzania wakati wa Mashindano ya Dunia ya Mpira wa Miguu yaani FFA World Cup yatakayofanyika nchini Marekani kati ya mwezi Juni na Julai mwaka 2026.
Kupitia mashindano hayo Tanzania itashirikisha wadau muhimu wakiwemo watangazaji mashuhuri wa michezo duniani na kujitangaza kupitia mabango ya kiijitali “billboards” yatakayowekwa katika maeneo ya kimkakati nchini Marekani.

Katika kuongeza hamasa ya kufuatiliwa na watu wengi zaidi kwenye mitandao ya kijamii duniani, Wizara itatumia watu maarufu na wenye ushawishi mkubwa kama vile wanamichezo ili kuendelea kujitangaza kwa kuwaleta kutembelea maeneo yenye vivutio vya utalii.
Kupitia watu hao maudhui mbalimbali yenye kulenga kuitangaza Tanzania yatarekodiwa na kurushwa kwenye tovuti mbalimbali sambamba na mitandao ya kijamii ya watu hao kama vle Instagram, LinkedIn, Tiktok, Facebook na mtandao wa X.

