Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umewataka makandarasi wote wanaotekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara kuhakikisha wanazilinda, kuziimarisha na kuzitunza njia mbadala ili ziweze kupitika wakati wote, hususan kipindi cha mvua kubwa.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma, Catherine Sungura, imesisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuzuia kufungwa kwa barabara, kupunguza msongamano wa magari na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa miundombinu ya barabara unaendelea kuzingatiwa wakati miradi ya maendeleo ikiendelea kutekelezwa.
Catherine amesema makandarasi wote wanapaswa kuhakikisha njia mbadala zinazotumika wakati wa ujenzi zinakuwa imara na zinapitika wakati wote bila kusababisha usumbufu kwa wananchi.
“Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa, bado kuna miradi ya maendeleo ya barabara inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa mifereji ya maji, makaravati, barabara za zege pamoja na maandalizi mengine ya kiufundi katika maeneo tofauti ya miradi,” amesema.
Aidha, TARURA imewataka makandarasi kuweka mifumo madhubuti ya kupitisha maji ya mvua katika njia mbadala ili kuzuia uharibifu wa miundombinu na kuhakikisha magari yanaendelea kupita kwa usalama na urahisi wakati wote.
Wakala huo umesisitiza kuwa usimamizi makini wa miradi hiyo ni muhimu ili kuhakikisha maendeleo ya miundombinu hayaathiri huduma za usafiri kwa wananchi, hasa katika kipindi cha mvua zinazoendelea kunyesha.

