Na Mwandishi Wetu
MOROGORO: WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewataka wataalamu wa ubunifu wa majengo na ukadiriaji nchini kutumia taaluma zao kubuni miradi ya kisayansi yenye gharama nafuu na tija kwa maendeleo ya sekta ya ujenzi.
Akifungua Semina ya Mafunzo Endelevu na maonesho ya vifaa vya ujenzi yaliyoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji (AQRB) mkoani Morogoro, Ulega amesema ubunifu ni nguzo muhimu katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa.
Ameeleza kuwa mataifa yanayopiga hatua ni yale yanayowekeza katika ubunifu unaopunguza gharama huku ukiongeza ufanisi, hivyo kuwahimiza wataalamu kuendelea kujifunza na kuboresha ujuzi wao ili kuongeza tija katika kazi zao.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za upangaji miji na usanifu bora wa majengo ili kuongeza ushindani wa nchi na kuvutia uwekezaji pamoja na kukuza sekta ya utalii.
Pia amewakumbusha kuzingatia Sheria ya AQRB Sura ya 269 ili kuhakikisha ubora na usalama wa majengo.
Ulega amewataka wataalamu kutoa huduma kwa weledi ili jamii itambue tofauti kati ya wataalamu waliosajiliwa na wasiothibitishwa, huku akiwahamasisha kujitangaza zaidi ili kujenga heshima ya taaluma zao.

Akizungumzia ubunifu wa wanafunzi katika maonesho hayo, amesema ameridhishwa na mawazo yao na kusisitiza kuwepo mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa ubunifu unaoendana na teknolojia.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa AQRB, Dkt. Daniel Matondo, amesema wataendelea kusimamia taaluma hiyo kwa kuimarisha ubunifu na ushindani.
Naye Rais wa Chama cha Wabunifu Majengo Tanzania, Mecky T’chawi, ameahidi kushirikiana na serikali kuendeleza sekta hiyo kwa viwango vya kisasa.

