Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Viti Maalum, Dkt. Neema Majule, ameitaka Serikali kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kwa kuwapatia elimu ya fedha, ujasiriamali na mitaji ili waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.
Akichangia hotuba ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, bungeni Dodoma, Dkt. Majule amesema wanawake wanahitaji zaidi ya motisha; wanapaswa kufundishwa namna ya kubuni na kuendeleza mawazo ya biashara pamoja na kupata mifumo rahisi ya kuwasaidia kuanzisha na kukuza miradi yao.
Amepongeza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne, sekta ya elimu imepiga hatua kubwa kutokana na ujenzi wa madarasa zaidi ya 78,000 na shule nyingi za kisasa hata vijijini.
Amesema hatua hiyo imeondoa changamoto ya wanafunzi kusoma katika mazingira duni.
Aidha, ameisifu Serikali kwa kuboresha sekta ya afya kwa kujenga zahanati katika vijiji, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa na rufaa, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa vifaa tiba.
Kuhusu uchumi, amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua kuelekea uchumi wa kati wa juu, lakini amesisitiza umuhimu wa uchumi shirikishi unaowahusisha wanawake na wanaume katika sekta zote, ikiwemo kilimo na sekta binafsi.
“Maendeleo haya hayawezi kuwa endelevu bila ushiriki wa wanawake. Wanawake washirikishwe kuanzia kupanga, kutekeleza hadi kutathmini miradi ya maendeleo,” amesema.
Dkt. Majule amesisitiza umuhimu wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, akitaka usimamizi na ufuatiliaji wake uimarishwe ili kuhakikisha wanawake wananufaika ipasavyo.
Pia amezungumzia Sh. Bilioni 200 zilizotengwa kwa ajili ya wajasiriamali, akitaka ziwanufaishe walengwa kwa kuwepo utaratibu mzuri wa utoaji wake.
Ameongeza kuwa pamoja na mitaji, wanawake wanahitaji masoko ya uhakika ya bidhaa zao, hivyo akashauri kuwepo mifumo ya kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza tija na kipato.

