Na Lucy Ngowi
Dodoma: MBUNGE wa Bukoba Mjini, Johnston Mtasingwa, amesema zaidi ya wafanyabiashara wa senene 1,000 katika jimbo lake hawana eneo rasmi la kufanyia shughuli zao, hali inayowalazimu kufanya biashara pembeni mwa eneo ambalo kwa sasa linajengwa jengo la kituo cha mabasi.
Akizungumza bungeni leo Januari 30, 2026, Mtasingwa aliitaka serikali kutenga fedha za ziada ili kupanua jengo hilo na kuweka eneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara hao wa senene.
Pia aliomba Waziri husika kutembelea jimbo la Bukoba Mjini ili kujionea hali halisi na kupata fursa ya kuzungumza na wafanyabiashara hao.
“Je, serikali haiwezi kuongeza fedha kidogo kwenye mradi huo ili hawa wafanyabiashara wapate sehemu sahihi ya kufanyia shughuli zao? Na ni lini Mheshimiwa Waziri ataambatana na mimi kwenda kuona maeneo hayo na kuzungumza na wafanyabiashara wa Bukoba Mjini?” alihoji Mtasingwa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo, alisema serikali kwa kushirikiana na Manispaa ya Bukoba imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa soko la senene katika eneo la Soko la Mjini, maarufu kama Senene Complex.
Alisema lengo la mradi huo ni kuwakusanya wafanyabiashara wote wa senene katika eneo moja na kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira rafiki na salama.
Aliongeza kuwa suala la uwezeshwaji wa wafanyabiashara linaendelea kuratibiwa kupitia serikali za mitaa, na kwa kuwa nchi inaelekea katika mchakato wa bajeti, ni matarajio ya serikali kwamba ombi hilo litaingizwa rasmi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.
“Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha serikali inaweka msukumo wa kutosha katika utekelezaji wa mradi huu,” alisema Londo, huku akithibitisha kuwa baada ya shughuli za Bunge, ataambatana na Mbunge Mtasingwa kutembelea jimbo la Bukoba Mjini.

