Na Lucy Ngowi
TANGA: bAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imesisitiza kuwa bima ni nyenzo muhimu ya kulinda maisha ya wananchi na uchumi wa taifa, na si jambo la hiari kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidhani.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea mkoani Tanga kuanzia Januari 19 haLupilyamwaka huu 2026, Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya, amesema bima ina mchango mkubwa katika kulinda shughuli za kilimo,
Biashara na uzalishaji, pamoja na kupunguza athari za majanga kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa baada ya Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, kutembelea banda la TIRA katika maadhimisho hayo.
Dkt. Lupilya amesema TIRA haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya makampuni ya bima yatakayokiuka miongozo, sheria na taratibu zilizowekwa, akisisitiza kuwa ukiukwaji wa sheria hizo unakwamisha ukuaji wa sekta ya bima na maendeleo ya uchumi wa taifa.
Ameeleza kuwa mamlaka hiyo, kwa kushirikiana na makampuni ya bima, inaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa wa masuala ya bima, akibainisha kuwa ukosefu wa elimu hiyo hulazimisha serikali kubeba mzigo mkubwa wa kifedha unaotokana na majanga, umaskini na mdororo wa uchumi.
“Endapo taifa halitaelimishwa kuhusu umuhimu wa bima, serikali italazimika kugharamia athari za majanga, umaskini na kushuka kwa shughuli za uzalishaji, hali inayoliletea taifa mzigo mkubwa wa kiuchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa juhudi za TIRA na makampuni ya bima katika kutoa elimu kwa umma ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha ukuaji wa pato la taifa na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Sambamba na hilo, amezitaka kampuni za bima kuwa wabunifu katika kubuni bidhaa zinazokidhi mahitaji halisi ya wananchi, badala ya kuangazia zaidi maslahi ya makampuni yenyewe.

