Na Mwandishi Wetu
DODOMA: MWENYEKITI wa Kijiji cha Makanda-Mvumi, Msafiri Makacha, ameiahidi kuendelea kufuatilia mgogoro wa shamba la Sayu Seni, mkazi wa Wilaya ya Bahi, aliye nyang’anywa shamba na mali zake na Nzije Shanga.
Amesema hatua hizo zitahakikisha kila upande anapata haki, licha ya kutokuwa na ufahamu wa kutosha ikiwa mlalamikiwa na mlalamikaji walishalizana awali.
Makacha amesema mgogoro huo umetokana na udugu na sintofahamu kimaamuzi.
Kauli hiyo inajiri baada ya Seni kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuingilia kati.
Seni ameeleza kuwa kitendo cha kumnyang’anya shamba na mali zake, pamoja na vitisho kwa familia yake, kimesababisha kukimbia na kubaki peke yake bila kujua atakayeishi.
Amesema vitendo hivyo vya uonevu vimemuathiri kiuchumi, kijamii na kisaikolojia, na kumfanya ashindwe kuhudumia familia yake.
Seni alisema, “Niliamia Bahi mwaka 2009 baada ya kununua shamba kutoka kwa Buda na Msalali.
“Mwaka 2017 nilipanua shamba hadi hekari 10 kwa kilimo. Nilipojaribu kufuata taratibu za kibali chenye Sh. 5,000, niliambiwa natozwa faini ya Sh. 300,000, ambayo sikukuwa nayo, hivyo kuanza matatizo.”
Kwa upande wake, Nzije Shanga amedai yeye ndiye mmiliki wa eneo hilo na alipewa na uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na kijiji, lakini hakutaka kutoa maelezo zaidi akisema anashughulika na kilimo na ufugaji.

