Na Danson Kaijage
DODOMA: CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Taifa kimetaja changamoto saba kuu zinazowakabili watumishi wa umma, zikiwemo kucheleweshwa kwa malipo ya stahiki, mifumo ya kiutumishi na masuala ya heshima kazini.

Akisoma risala mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Deus Sangu, wakati wa ufunguzi wa kikao cha 31 cha Baraza Kuu la TALGWU Taifa jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Wandiba Ngocho, amesema changamoto kubwa ni kutolipwa kwa wakati fedha za likizo kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ameeeleza kuwa utaratibu wa kulipa fedha hizo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri umesababisha watumishi wengi kucheleweshewa malipo, wengine tangu mwaka 2018.
TALGWU imeiomba Serikali itenge bajeti ya likizo kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali, kama ilivyo kwa watumishi wa kada ya ualimu.

Changamoto ya pili ni malipo ya leseni za kutoa huduma kwa watumishi wa kada ya afya, ambapo wamekuwa wakilazimika kujilipia ada hizo binafsi.
TALGWU imependekeza waajiri walipe ada hizo na leseni hizo zisitumike kama kigezo cha kupandishwa madaraja.
Ngocho pia alilalamikia tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwadhalilisha watumishi wa umma hadharani, hasa wakati wa ziara za ukaguzi wa miradi.
Alisema hatua hiyo hushusha morali ya kazi na kuharibu taswira ya utumishi wa umma, akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria na kiutawala.

Changamoto nyingine ni kutolipwa kwa wakati stahiki za uhamisho, licha ya maelekezo ya Serikali kutowahamisha watumishi bila bajeti.
Aidha, TALGWU ilibainisha changamoto katika matumizi ya mfumo wa upimaji wa utendaji kazi (PEPMIS), ikiiomba Serikali kuongeza elimu kwa watumishi na wasimamizi wao.
Kwa upande wa miundo ya utumishi, chama kilieleza kuwepo kwa matatizo ya kubadilishiwa vyeo kwa kada zisizo za walimu, bila kuzingatia uzoefu wa mtumishi.
Pia kiliomba shahada ya uzamili iwe kigezo cha nafasi za uteuzi, si sharti la kimuundo.
Changamoto ya saba ni kutokuhuishwa kwa wakati Mabaraza ya Wafanyakazi, ambapo hadi Desemba 2025, mabaraza 60 kati ya 197 yatakuwa yameisha muda wake.
TALGWU imemuomba Waziri kuwaelekeza waajiri kutekeleza matakwa ya kisheria.

