Na Mwandishi Wetu, Njombe
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza wafanyakazi waliofanya vizuri na kutunukiwa zawadi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) 2026, yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe.
Katika hafla hiyo, Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA) kiliwatambua wanahabari sita kwa umahiri wao.
Miongoni mwa waliopata tuzo ya kitaifa ni Idda Mushi wa ITV na Radio One, aliyekabidhiwa tuzo na Rais Samia, pamoja na mwandishi mwandamizi Lucy Ngowi wa Gazeti la Mfanyakazi.

Wanahabari wengine waliotambuliwa na JOWUTA ni Alfred Zakaria (The Respondents), Tamali Vullu (Mwananchi – Dar es Salaam), Ashura Ibrahim Kazinja (Mtanzania Digital – Morogoro) na Rashid Mtagaluka (Pambazuko).
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Rais Samia amewataka wafanyakazi nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi kadri uchumi unavyoruhusu, huku akiahidi hatua zaidi za kuimarisha ustawi wa wafanyakazi.
“Ndugu zangu chapeni kazi, Serikali ipo, inawasikiliza na inawathamini. Tushirikiane na kutanguliza maslahi ya Taifa,” amesema.
Aidha, Rais Samia ameonya kuwa tofauti zisigeuke chanzo cha kuvuruga amani, akisisitiza umuhimu wa umoja, mshikamano na utulivu kwa maendeleo ya Taifa.
Awali, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamuhokya, amesema wafanyakazi wataendelea kushirikiana na Serikali kuboresha mazingira ya kazi.
Amemshukuru Rais kwa kuongeza mishahara na kushughulikia madai ya wafanyakazi, ikiwemo zaidi ya Sh. Bilioni mbili zilizotolewa kulipa madeni ya wafanyakazi wa TAZARA.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba aliwataka wafanyakazi kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutatua changamoto mbalimbali na kuboresha uchumi.
Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma, amesema chama hicho kimeshiriki kwa mara ya kwanza katika maadhimisho ya Mei Mosi na kimeanza kutoa tuzo kwa wanahabari.
Ameongeza kuwa mwaka ujao wataongeza wigo wa tuzo na kutoa mafunzo kwa wanachama, ikiwemo masuala ya bima ya afya na uwekaji akiba.

