Na Lucy Lyatuu
KAMATI Kuu ya Chama Cha ADA -TADEA kimewavua uanachama wanachama wake kutokana na kukiuka taratibu mbalimbali za chama hicho huku wakijaza nafasi zilizokuwa wazi.
Waliovuliwa uanachama ni pamoja na aliyekuwa mgombea mwenza chama hicho, Ali Makame Issa, Katibu wa Baraza la Vijana, Alphonce Mayunga na Katibu Mkoa wa Mwanza, Deusdedit Tiba.
Katibu Mkuu wa ADA_TADEA, Salehe Msumari amesema hayo leo Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari na kuongeza kuwa baada ya chama kujaza nafasi za viongozi hao watapeleka taarifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Amesema wagombea hao wamevuliwa uanachama kwa sababu mbalimbali na kwamba kuanzia sasa matamko ambayo yamekuwa yakitolewa na aliyekuwa mgombea mwenza hayatatambuliwa na chama hicho.
Amesema nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar imechukuliwa na Ally Mohamed kutokana na aliyekuwepo kuhamia chama kingine cha siasa.
Amesema pia wamejaza nafasi nyingine Makamu Mwenyekiti Bara, ambaye ameumwa muda mrefu sana na nafasi hiyo kukaimishwa kwa Farida Abdallahna Katibu Mkuu Mwenezi ambaye alihama chama hicho na nafasi yake kuchukuliwa na Mwenyekiti mkoa wa Simiyu, Luhende Kassim, na nafasi ya Katibu wa Vijana kuchukuliwana Suzan Thomas.
Kuhusu uchaguzi amesema chama hicho hakijapata nafasi yoyote ya uongozi na kwamba Kamati hiyo imekutana kujadili kuona walipokosea na kuwa na mapendekezo ndani ya chama ya nini kitakachofuatwa.
Kuhusu hotuba ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati akizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyekiti wa Chama hicho, Juma Ali Khatib amesema wanapongeza kwa hotuba nzuri hususani alipotoa msamaha kwa walioshiriki katika vurugu za Oktoba 29, siku ya uchaguzi.

Amesema pia Kamati hiyo inapongeza uundwaji wa Wizara maalum ya Vijana ambayo itagusa mambo mengi yanayohusu kundi hilo.
Khatib amewataka pia vijana kuepukana na hamasa zinazosababisha kushiriki kwenye maandamano kwa kuwa ni eneo lililoitia doa Tanzania .


