Na Lucy Ngowi
WAZALISHAJI, wafanyabiashara na wakaangaji wa kahawa duniani wamealikwa kushiriki Kongamano na Maonyesho ya 21 ya Kahawa bora Afrika, yatakayofanyika Dar es Salaam, Februari 26 hadi 28 mwaka ujao 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo amesema hayo katika mkutano wa maandalizi ya kongamano hilo ulioandaliwa na bodi hiyo kwa kushirikiana na Chama cha Kahawa Bora za Afrika (AFCA).
Kimaryo amesema kongamano hilo linatoa fursa ya pekee kwa nchi ya Tanzania baada ya kufunguka kibiashara.
“Tanzania sasa uzalishaji wetu wa kahawa unaendelea kuongezeka,imekuwa ni fursa kwetu kuona ni namna gani tunaileta tena dunia ya kahawa hapa nchini.
“Kwa hiyo hii ni fursa pekee kwa wakulima wa kahawa na wadau wote wa sekta ya kahawa Tanzania kuionyesha ni namna gani tunavyoweza kupata masoko mapya, kutafuta masoko na kuonyesha kahawa zetu zote mbili ambazo ni Robusta na Arabica,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya AFCA, Amir Hamza amesema kilichoipa nguvu ya kuleta maonesho hayo Tanzania, ni kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuifungua nchi kibiashara.
“Huu ni wakati sahihi wa wakulima kuonyesha ni nini inafanya katika kahawa kwa dunia,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko TCB, Frank Nyarusi amesema zaidi ya wakulima wadogo 320,000 wanategemea kahawa hapa nchini, pia watu milioni mbili wanaitegemea kahawa katika maeneo mbalimbali.
“Kahawa inaingiza dola za marekani mil 200 ni chanzo kikubwa cha mapato katika nchi,” amesema.
Amesema jitihada wanayoifanya ni kushirikisha wadau katika mnyororo wa kahawa, pia kutengeneza mazingira wezeshi ili kila mtu awekeze, auze na kufurahia fursa zote zilizopo kwenye kahawa.