Na Mwandishi Wetu
SEKTA ya Maji inazidi kushirikisha wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya maji yenye manufaa kwa jamii.
Moja ya wadau hao ni kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola, ambayo imewekeza Dola za Marekani milioni 1.94 katika mradi wa uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Kidakio cha Ngerengere, Bonde la Wami-Ruvu, mkoani Morogoro.

Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji, Rosemary Rwebugisa, amesema mradi huu unalingana na mkakati wa Wizara wa kuimarisha uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali hiyo kwa maendeleo ya jamii na uchumi.
Wakulima na maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro, Mvomero, na Morogoro Vijijini watafaidika kutokana na kulindwa kwa chanzo hicho muhimu kinachohudumia Mkoa wa Pwani na Jiji la Dar es Salaam.
Rwebugisa ameongeza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, sekta binafsi, na jamii katika miradi ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, sambamba na kukuza uelewa wa matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za serikali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha usalama wa maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu, Juvenalis Tarimo, amesema taasisi hiyo itaendelea kusimamia rasilimali za maji kwa kuzingatia sheria za usimamizi wa rasilimali hizo ili kuhakikisha mradi unaleta tija kwa jamii.
Mradi utatekelezwa katika Ngerengere, ukijumuisha kujenga uwezo kwa jamii katika usimamizi endelevu wa maji na kuhamasisha mbinu bora za kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Mradi unaongozwa na Shirika la Global Water Challenge (GWC), International Union for Conservation of Nature (IUCN), Coca-Cola Tanzania, na Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu, ukiwa sehemu ya jitihada za pamoja za kulinda vyanzo vya maji na kuimarisha maisha ya wananchi.

