Na Lucy Ngowi
DODOMA: WAZAZI na walezi wameshauriwa kupeleka watoto katika Chuo cha Ufundi cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kujifunza useremala waweze kujiajiri na kuajiri wengine ili kujipatia kipato.
Mwalimu wa Fani ya Useremala kutoka Chuo cha VETA, mkoani Tanga Yusufu Mkahala amesema hayo kwenye maonesho ya wakulima, wafugaji na Wavuvi yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema useremala ni fani mama kwa kuwa mahitaji yake ni mengi kwa matumizi katika jamii, hivyo uhitaji ni mkubwa hasa wa samani kuanzia nyumbani ,shuleni hadi maofisini.
“Katika useremala unaweza kuzaliwa maskini lakini siyo lazima kufa maskini kwa sababu ukiwa na fani hiyo una uwezo wa kufanya kazi bila oda ya mtu yeyote na ukabuni kitu kizuri chenye mvuto kwa watu na watu wakanunua,” amesema.
Amesema mtu akiwa na fani hiyo ni rahisi kujiajiri na kwamba anapopata wateja wengi zaidi ni rahisi kuajiri wengine ili kukamilisha kazi za wateja alizo nazo.
Amesema fani hiyo ni muhimu katika kutatua changamoto ya ajira kwani uwezekano wa kujiari,kuajiriwa ama kuajiri wengine ni mkubwa.