Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WANAWAKE wa Umoja wa Taasisi za Kimataifa za Utafiti (CGIAR), wakiongozwa na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA), wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wanawake waliojifungua, madaktari na manesi katika Kituo cha Afya Kawe.
Taasisi nyingine zilizoshiriki ni Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga (IRRI) na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Ubunifu katika mnyororo wa thamani ya uvuvi (WorldFish)
Ofisa Mawasiliano wa IITA, Gloriana Ndibalema amesema kwamba wanawake wa umoja huo ambao wanafanya utafiti wa kilimo wameamua kutoa msaada huo kutokana na michango waliyoichanga katika sekta ya afya kwenye wodi ya wazazi ya Kituo cha Afya Kawe ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
“Tunafanya utafiti wa kilimo nchi za kiafrika, katika Afrika Mashariki tunafanya utafiti Kenya, Tanzania, Uganda, Madagasca, Comoro.
“Tunafanya utafiti wa mihogo mahindi soya, jamii ya mbaazi, ndizi. Utafiti wetu tunaanzia maabara mpaka mnyororo mzima wa thamani,” amesema.
Amesema wameweza kutoa kompyuta mbili kwa ajili ya kituo hicho cha afya, vipimo vya mapigo ya moyo wa mtoto, mapazia, mipira wanayotumia wanawake wakijifungua, vitenge kwa ajili ya wazazi na madaktari na wauguzi, pamoja na vitambaa vya suruali kwa ajili ya watumishi wa wodi hiyo.
Vile vile wametoa mabeseni yaliyowekwa vifaa mbalimbali kwa ajili ya mtoto na mama kwa wazazi waliojifungua, walioruhusiwa kwenda nyumbani, walioko hospitalini na wanaotarajiwa kujifungua.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho cha Afya, Dkt. Isack Mbalwa ameshukuru kwa msaada huo uliotolewa na umoja huo wa wanawake, kwa kusema kuwa wanawake ni nguzo muhimu.
“Kwa zawadi hii mmewagusa na kuwafariji wamama hawa,” amesema.
Pia amesema kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali, mwanzo kilikuwa ni zahanati lakini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuongeza fedha waliongeza maabara, jengo la wama na jengo la kulaza wagonjwa.
“Kituo hiki kinatoa huduma ya kinywa na meno, wagonjwa wanaohudumiwa na kurudi nyumbani, matunzo kwa wenye ukimwi, kujifungua mama na mtoto pamoja na upasuaji,” amesema.
Naye muuguzi katika wodi hiyo ya wazazi Aisha Said ameshukuru wanawake hao kwa msaada walioutoa kwani ni wachache wenye moyo huo, wapo walio na uwezo lakini hawatoi msaada kama huo.
Mzazi Mar Mfikwa naye alishukuru umoja huo kwa upendo waliouonyesha kwao wazazi kwa kuwapatia mabeseni ya kuogeshea watoto pamoja na vifaa vingine mbalimbali.