Na Lucy Ngowi
RUVUMA: WAMILIKI, Waendeshaji wa Migodi, Vituo vya Kuuzia na Kuhifadhia Makaa ya Mawe wamepewa siku 30, wawe wanasajili miradi yao ili kupata vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM).
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limetoa muda wa usajili huo na uhakiki kuanzia Disemba nane mwaka huu, 2024
Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria wa NEMC, Jamal Baruti ametoa agizo hilo kutokana na ukaguzi uliofanyika katika vitalu mbalimbali vya migodi na kubaini makosa yanayokiuka Sheria ya usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004.

Agizo hilo amelitoa alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Mkoa wa Ruvuma mara baada ya kukamilisha ukaguzi huo.
Ametaja makosa yaliyoonekana kuwa ni kutofanyika kwa Tathmini ya Athari za Mazingira (TAM), ukosefu wa mifumo ya usimamizi wa mazingira, kutelekezwa kwa migodi pasipo kukarabati mazingira na uchafuzi wa vyanzo vya maji na hewa.
Pia kuongeza mawanda ya shughuli za migodi bila taarifa na idhini ya kisheria, kukosekana kwa taarifa za Upelembaji za kila mwaka na kukosekana kwa mipango ya urejeshaji Mazingira.
Amesema ukaguzi huo uliofanywa na timu ya wataalam kutoka NEMC kwa kushirikishana na wamiliki wa migodi umefanyika katika migodi 16 kati ya 18, maeneo ya biashara za makaa ya mawe saba kati ya 15 na maeneo mawili ya utafiti kuanzia Novemba 27 hadi Desemba nane, mwaka huu 2024 katika Wilaya za Madaba, Songea, Nyasa na Mbinga Mkoani Ruvuma.

Amesema timu hiyo pia imetoa elimu elekezi kwa wamiliki wa migodi ikiwemo kuweka miundombinu ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira, na ukarabati endelevu wa mazingira,
Baruti amesema baraza hilo litaendelea kutoa maelekezo na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wamiliki wa migodi ili kuhakikisha uzingatiaji wa Sheria na utekelezaji maagizo yaliyotolewa.
Pia kuchukua hatua za kisheria kwa wadau wote watakaoshindwa kutekeleza maelekezo hayo ikiwa ni pamoja na kupewa adhabu au kusimamisha shughuli zao ili kulinda Mazingira, afya ya jamii na kuhakikisha uwiano wa maendeleo ya kiuchumi, uhifadhi wa Mazingira na rasilimali za taifa.
