Na Mwandishi Wetu
WAKULIMA Mkoani Kagera wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza mavuno na kujiimarisha kiuchumi.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa wakati wa kampeni wa Kilimo ni Mbolea wilayani Misenyi.
Mkuu huyo wa mkoa amesema, hivi sasa bei ya Kahawa imeongezeka, lakini bila kuzingatia matumzi sahihi ya Mbolea mavuno yatakua kidogo na uimara wa bei hiyo sokoni hauwezi kumnufaisha mkulima.
Amesema matumizi sahihi ya mbolea kwenye mazao yanamsaidia mkulima kupata uhakika wa mavuno yake na hivyo kuwa na uhakika wa soko kutokana na mavuno yenye ubora atakayovuna.
“ Unapotumia mbolea kwa usahihi unapata uhakika wa mavuno yenye ubora yatakayo kupa bei nzuri sokoni na hivyo kujiongezea kipato chako binafsi na pato la taifa kwa ujumla wake”,amesema.
Vile vile amesema Serikali imetatua changamoto ya makali ya bei ya mbolea kwa kuleta mpango wa mbolea ya ruzuku unaosimamiwa na TFRA ili kila mkulima asajiliwe na kunufaika na mpango huo.
“Ndugu zangu wakulima niwakumbushe kuwa Serikali yetu imetatua changamoto ya bei ya mbolea kwa kuleta mpango wa mbolea ya ruzuku unaotekelezwa nchi nzima na ni haki ya kila mkulima kujisajili na kunufaika na bei himilivu ya ruzuku ” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA Dkt. Anthony Diallo, amesema mamlaka inahimiza matumizi sahihi ya mbolea kupitia majukwaa mbalimbali hivyo ni jukumu la kila mkulima kuitumia elimu wanayopewa na kuketa mabadiliko katika kilimo chao.
Dkt. Diallo amesema wakulima wa Kagera wanalima mazao mbalimbali ya chakula na biashara lakini hawatumii mbolea ipasavyo hivyo kujipunguzia kiasi cha mavuno ambayo wangstahili kuvuna iwapo wangetumia mbolea kwa usahihi.