Na Lucy Ngowi
MBEYA: DAKTARI wa Mifupa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dkt. Angela Mlingi, amesema wamehudumia jumla ya wagonjwa 472, ambapo wengi wao wamebainika kuwa na changamoto za kiafya kwenye maeneo ya mgongo na nyonga.
Dkt. Angela amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari katika Mqadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayomalizika Oktaba 14, 2025.

Amesema kati ya wagonjwa hao 472, takriban 40 wamependekezwa kufika MOI, Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya kina kutokana na hali zao za kiafya kuhitaji utaalamu zaidi.
Amesema wagonjwa wenye hali ya wastani wameelekezwa kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya kwa matibabu, huku Daktari huyo akieleza kuwa hospitali hiyo sasa ina uwezo mkubwa wa kutoa huduma za tiba ya mifupa baada ya madaktari wake kupatiwa mafunzo na MOI.
“Tunawashukuru wananchi kwa namna walivyojitokeza na kufurahia huduma. Hii inaonesha kuwa kuna uhitaji mkubwa wa elimu kuhusu afya ya mifupa, hasa ukizingatia kwamba watu wengi hupuuzia dalili za awali za maumivu kwa sababu ya uelewa mdogo,” amesema.

Ametoa wito kwa wananchi kujenga mazoea ya kufanya mazoezi mara kwa mara na kufika hospitalini pindi wanapohisi mabadiliko yoyote ya kiafya badala ya kusubiri hali kuwa mbaya.
“Wagonjwa wengi wanajua kuwa wanaumwa lakini kufuata huduma hospitalini imekuwa changamoto. Tunawahimiza watu wakapime afya zao mapema ili kama kuna tatizo, litibiwe kwa wakati,” amesema.