Na Lucy Ngowi
MBEYA: CHUO cha Ufundi Stadi (VETA) Mbeya kiimeonyesha teknolojia ya kisasa ya mfumo wa Hybrid kwa magari katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana yalnayoendelea mkoani humo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwanafunzi Adam Akyoo amesema teknolojia hiyo, inayowezesha gari kuendelea kuendeshwa kwa kutumia umeme hata mafuta yanapokwisha, inalenga kupunguza gharama za uendeshaji wa magari na kutoa suluhisho la muda mfupi kwa wamiliki wa magari ya kisasa yanayotumia nishati mchanganyiko.
“Tumewasilisha mfumo huu kama sehemu ya mafunzo tunayotoa kwa vijana wetu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia, hasa kwenye sekta ya usafiri ambayo sasa inategemea magari ya umeme,” amesema.
Amesena mfumo huo wa Hybrid unaunganisha mota ya umeme kwenye injini ya gari, ambapo umeme huzalishwa na kusaidia kuendesha gari hata mafuta yanapokosekana. Hii husaidia kupunguza utegemezi mkubwa wa mafuta, hasa maeneo ya mbali ambapo vituo vya mafuta ni vichache.
“Kuna ongezeko kubwa la magari ya umeme nchini, lakini mafundi wengi hawana ujuzi wa kuyashughulikia. Hii ni fursa kwa vijana kujifunza na kuwa sehemu ya suluhisho,” amesena..

Kwa upande wake Ofisa Habari na Uhusiano wa VETA Taifa, David Mpondyo, amesema VETA kwa sasa imeongeza nguvu katika kufundisha fani zinazohusiana na teknolojia mpya, ili kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanakuwa na ujuzi unaohitajika katika soko la sasa na la baadaye.
“Zamani tulikuwa tunafundisha zaidi magari ya dizeli na petroli, lakini sasa tunajikita kwenye magari ya umeme kwa kuwa ndiko dunia inaelekea. Tunataka vijana wetu wasipitwe,” amesema Mpondyo.
Amesema Kwa sasa, VETA ina zaidi ya vyuo 80 nchini, huku serikali ikitekeleza mpango wa ujenzi wa vyuo 65 vipya katika kila wilaya. Lengo ni kuongeza fursa kwa vijana wengi zaidi kupata mafunzo ya ufundi stadi kwa gharama nafuu, na kujiajiri au kuajiri wengine.
Amesema Katika baadhi ya vyuo kama VETA Dodoma na VETA Moshi, tayari kozi za kisasa kama uuzaji, ukarabati wa magari ya umeme, na welding ya viwango vya kimataifa zimeanzishwa ili kukidhi mahitaji ya miradi mikubwa kama vile bomba la mafuta la Afrika Mashariki (EACOP).
Mpondyo amehimiza vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na VETA kwa kuwa ndizo msingi wa ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
“Kama hujaweza kufika chuoni, fika kwenye maonesho haya. Hapa utajionea kazi za mikono ya vijana wenzako na kujua namna ya kujiunga. Elimu ya ufundi si suluhisho la waliokosa, bali ni msingi wa maisha ya kisasa,” amesema.