Na Lucy Lyatuu
DAR ES SALAAM: TAASISI ya uwekezaji nchini UTT AMIS imezindua kampeni ya elimu kwa umma ijilikanayo kama ‘Kijiwe Mchongo’ ikilenga kuelimisha masuala ya uwekezaji kwa jamii na rika zote namna ambavyo masoko ya fedha na mitaji yanavyoweza kuwanufaisha kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja.
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa taasisi hiyo Daud Mbaga, amesema hayo leo Dar es Salaam na kuongeza kuwa elimu hiyo itatolewa sehemu mbalimbali nchini na kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya taasisi hiyo.
“Uzinduzi wa kampeni hii inalenga kuhamasisha wananchi kuwekeza kupitia taasisi hiyo kwamba tuwafikie wananchi popote walipo kupitia majukwaa tofauti kama Youtube, instagram, facebook nahata redio,” amesema.
Amesema kampeni itasaidia wenye vipato vya chini, kati na juu wakutane sehemu moja kupitia UTT AMIS na waweze kuwekeza kwenye masoko ya fedha ambayo ni ya mitaji na fedha.
Amesema kijiwe mchongo ni kampeni ambayo watakwenda mtaa kwa mtaa, wakiongea na watu tofauti kujua ufahamu wao na kuwavuta kuingia kwenye mfiko na kama wapo waongeze uwekezaji.
Aidha amesema hadi sasa taasisi hiyo inasimamia fedha za watanzania zaidi ya Trilioni 2.2 na wawekezaji wapatao 340,000 na kwa miaka zaidi ya 20 imekuwa moja ya mifuko inayolipa gawio na faida kwa wawekezaji kila mwaka.
“Hivi sasa tuna mifuko sita ambayo ni umoja, wekeza maisha, watoto, kujikimu, ukwasi na hatifungani ambayo kwa pamoja mifuko hiyo imekidhi vigenzo vya ufanisi ambavyo ni usalama, faida, shindani na ukwasi,” amesema.
Ameongeza kuwa wastani wa faida katika mifuko kwa mwaka imekuwa kati ya asilimia 12 hadi 15 kulingana na hali ya soko.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Tasisi hiyo, Issa Waichinenda amesema katika kampeni inahamasisha wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwani ukiwekeza huko ni sehemu salama na kuna faida nzuri .
Amesema kiwango cha chini cha uwekezaji ni kuanzia sh 10,000 na uwekezaji naweza kuendelea kuweka kiwango chochote.