Na Lucy Ngowi
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imesema ina jukumu muhimu katika kusaidia kudhibiti magugu vamizi katika Ziwa Victoria kupitia matumizi ya njia za kibaiolojia kwa kutumia wadudu aina ya mbawakavu wanaokula gugu hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Meneja wa TPHPA Kanda ya Ziwa, Juma Mwinyimkuu, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi wakati wa Maonesho ya Kwanza ya Ziwa Victoria.
Amesema TPHPA imeshiriki maonesho hayo kutokana na wajibu wake wa kudhibiti magugu vamizi katika Ziwa Victoria, hususan gugu la Kariba ambalo mwaka jana liliongezeka kwa kasi na kusababisha changamoto kubwa katika ziwa hilo.
Mwinyimkuu amesema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika juhudi za kuondoa gugu hilo.
Aidha, mwishoni mwa mwaka jana 2025, timu ya wataalamu kutoka taasisi mbalimbali ilisafiri kwenda Uganda kujifunza namna nchi hiyo inavyodhibiti gugu hilo kwa kutumia mbinu za kibaiolojia.
Amesema baada ya mafunzo hayo, walirejea na wadudu aina ya mbawakavu wanaoshambulia gugu hilo na kukabidhiwa TPHPA kwa ajili ya kuendelea kuwazalisha.
“Hadi sasa tumefanikiwa kuzalisha zaidi ya wadudu 40,000. Baada ya kujiridhisha kuwa hawana madhara kwa mazingira, tuliwaweka katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria kwa ajili ya kupima ufanisi wao,” amesema Mwinyimkuu.
Ameeleza kuwa hatua inayofuata ni kuanzisha eneo maalumu la kuzalisha wadudu hao kwa wingi katika ukanda wa ziwa kabla ya kuwaachia rasmi ndani ya ziwa kwa ajili ya kudhibiti gugu hilo.
Mwinyimkuu amesema mafanikio ya mpango huo yanategemea ushirikiano wa wadau mbalimbali, hivyo TPHPA inaendelea kuwakaribisha taasisi na wananchi kushiriki katika utoaji wa elimu na ujenzi wa uwezo kwa jamii zinazozunguka Ziwa Victoria.
Amesema lengo ni kuunda vikundi vitakavyoshiriki kuzalisha wadudu hao na baadaye kuwaachia katika ziwa ili kusaidia kudhibiti kuenea kwa gugu la Kariba.

