Na Lucy Lyatuu,Dodoma
SERIKALI imesema licha ya kusogeza huduma za ugawaji wa vitambulisho karibu na wananchi, na kuanzisha huduma ya kutuma ujumbe mfupi kwa wananchi ambao vitambulisho vyao vimechapishwa kuwataka kufika katika ofisi za wilaya walizojisajili na kuvichukua, bado kuna vitambulisho 668,822 katika ofisi za wilaya za NIDA ambavyo havijachukuliwa.
Aidha, imesema NIDA inatarajia kuanza kufanya usajili wa watoto kuanzia umri wa kuzaliwa ili kutoa namba ya utambulisho ya kipekee ambayo itajulikana kama JAMII NAMBA.
Waziri wa Mambo Ya Ndani Ya Nchi, Patrobas Katambi amesema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo Bungeni na kuongeza kuwa NIDA imeanzisha namba maalum ya kutuma ujumbe mfupi bila malipo (sms) ambayo ni 15274.

Amesema wananchi wote waliopewa taarifa ya kuchukua vitambulisho vyao kujitokeza kwenda kuvichukua kwa kuwa vitambulisho hivyo vitawawezesha kupata utambulisho rasmi katika kupata huduma mbalimbali za kijami, kiuchumi na kiusalama ikiwemo Bima ya Afya,
“Namba hiyo itamuwezesha mwananchi kufuatilia hatua ya maombi ya kitambulisho cha Taifa ilipofikia pamoja na kupata namba yake ya utambulisho bila kulazimika kufika katika ofisi za NIDA,” amesema na kuwataka Wabunge kuwahamasisha wananchi katika maeneo yao kutumia namba 15274 kupitia simu.
Amesema katika kuhakikisha NIDA inakuwa na kanzidata yenye taarifa sahihi za watu, Serikali imetoa kibali maalumu cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Oktoba 2025 hadi Septemba 2026 cha kuruhusu wananchi waliotoa taarifa zisizo sahihi wakati wa usajili, kufanya mabadiliko ya taarifa hizo na kutoa taarifa sahihi.
Amesema hadi kufikia Aprili 2026 NIDA imepokea na kufanyia kazi maombi ya mabadiliko ya taarifa kutoka kwa wananchi 873 na kutoa rai kwa wananchi wenye changamoto ya taarifa zao katika mfumo wa NIDA kutumia fursa iliyotolewa ya kufanya maboresho ya taarifa zao na kuhakikisha taarifa wanazotoa ni sahihi.
Kuhusu namba kwa watoto amesema NIDA inatarajia kuanza kufanya usajili wa watoto kuanzia umri wa kuzaliwa ili kutoa namba ya utambulisho ya kipekee ambayo itajulikana kama JAMII NAMBA.
Amesema namba hiyo itatumika katika kupatiwa huduma mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kiusalama tangu mtu anapozaliwa hadi mwisho wa maisha yake.

