Na Lucy Lyatuu,Dodoma
KATIKA kutekeleza bajeti ya Wizara ya Viwanda Na Biashara kwa mwaka 2026/27 imeweka vipaumbele saba ambavyo ni pamoja na Kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati ya Viwanda.
Waziri wa Wizara hiyo, Judith Kapinga amesema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo Bungeni,ambapo Wizara inaomba kuidhinishiwa jumla sh bilioni 138.
Amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma kwa kuboresha mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kongani na mitaa ya viwanda kwa ajili ya viwanda vidogo na vya kati na Kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara kupitia ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa, elimu na mafunzo ya ujuzi.
Kapinga amesema vipaumbele vingine ni kuimarisha upatikanaji wa fedha na mitaji kwa wajasiriamali na wazalishaji viwandani, kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea ukuaji wa Sekta binafsi na kuendelea na utafutaji wa masoko kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini.

Amesema pia serikali itaanzisha na kuendeleza mawazo ya biashara na bunifu kwa vijana na kuanzisha vituo kwa vijana kwa lengo la kuchochea uchumi.
Amesema Vituo hivyo ni muhimu vitakavyowawezesha vijana wenye mawazo bunifu ya biashara kupata mazingira rafiki ya kubuni, kukuza na kuendesha biashara zenye ushindani katika soko la ndani na la kimataifa.
Aidha amesema katika kipindi hiki ambacho dunia inabadilika kwa kasi kupitia maendeleo ya teknolojia, uchumi wa kidijitali na matumizi ya maarifa, ni muhimu kwa nchi yetu kuwekeza katika ubunifu na ujasiriamali wa vijana.
Aidha, amesema kwasasa, mfumo wa biashara duniani umejikita katika huduma zinazotolewa kidijitali ambapo inategemewa mauzo ya biashara ya kidijitali yatakuwa mara mbili zaidi ya biashara ya bidhaa.

