Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano wa kikanda katika usimamizi wa rasilimali za maji wakati wa Mkutano wa Maji na Diplomasia ya Maji uliofanyika Bishoftu, Ethiopia.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji Juma Aweso, Mkurugenzi wa Ubora wa Maji, Heri Chisute, amesema mkutano huo wenye kaulimbiu ya diplomasia ya maji na ushirikiano wa kikanda kwa maendeleo endelevu unasisitiza kuwa maji si rasilimali tu bali ni uhai, daraja la kuunganisha mataifa na msingi wa amani na ustawi.
Ameeleza kuwa Tanzania imejifunza kupitia mifumo ya majishirikishi kama Bonde la Mto Nile, Zambezi, Songwe na Ziwa Victoria kuwa ushirikiano hubadili maji kuwa chanzo cha umoja badala ya migogoro.

Chisute amesema Tanzania inaongozwa na misingi mitatu, usawa na ujumuishi ili kila jamii ishiriki katika uamuzi, uendelevu na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali zisizo toshelevu, na diplomasia pamoja na ushirikiano unaojenga uaminifu na kupanua mazungumzo.
Ameongeza kuwa Tanzania na Ethiopia zina historia ya uhusiano mzuri, na mkutano huo unatarajiwa kuimarisha zaidi ushirikiano huo na kuchochea utawala endelevu wa maji.
Aidha, ametoa wito kwa nchi za Afrika kuunda mifumo wazi, jumuishi na inayotekelezeka ili rasilimali za maji ziwe chachu ya maendeleo na mshikamano wa kikanda.

Mkutano huo uliwakutanisha mawaziri, watunga sera na wataalamu kutoka nchi za Bonde la Mto Nile kujadili mbinu shirikishi za usimamizi wa maji, kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za utafiti na kuongeza ushiriki wa vyombo vya habari katika uelimishaji wa umma.
Diplomasia ya maji inahusisha matumizi ya mazungumzo na ushirikiano wa kisiasa kusimamia rasilimali za maji zinazovuka mipaka, kwa lengo la kuzuia migogoro, kukuza amani na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji.

