Na Mwandishi Wetu, Kampala, Uganda
TANZANIA imejipanga vema kuhakikisha inatumia fursa ya uwepo wa soko la pamoja la mauziano ya umeme kwa nchi wanachama wa soko la pamoja la nchi za Mashariki mwa Afrika ( EAPP ) .
Fursa hiyo ni pamoja na kuhakikisha inaunganisha miundombinu yake ya kusafirisha umeme na nchi wanachama wa EAPP.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko wakati wa mkutano wa 19 wa nchi wanachama wa umoja wa mauziano ya umeme EAPP uliowakutanisha Mawaziri wa Nishati na Makatibu Wakuu nchini Uganda.
Mkutano huo umezungumzia masuala mbalimbali ikiwemo kupitisha mabadiliko ya muundo wa kiuongozi wa EAPP, kuridhia kanuni na taratibu za kiuendeshaji za EAPP .
Kadhalika umeridhia uwepo wa kitengo huru cha masoko kinachojitegemea kusimamia soko la pamoja la mauziano ya Umeme kwa nchi wanachama.
‘”Nafurahi kuona kuwa tumefikia muafaka kwenye masuala ya msingi kwenye kikao cha Mawaziri wa Nishati hususani uwepo wa kitengo huru cha Masoko kinachojitegemea kwa ajili ya kusimamia mauziano ya umeme.
Na kwakuwa Tanzania tutakuwa na umeme kutoka mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere tutatumia vema fursa hiyo kuwauzia umeme nchi wanachama pale tutakapokuwa na ziada na sisi kununua tutakapokuwa na upungufu’’ amesema Dkt. Biteko.
Katika kufanikisha hilo Dkt. Biteko amesema tayari miundombinu wezeshi inaendelea kuwekwa kupitia Shirika la Umeme Tanzania TANESCO ili kujiandaa kuingia kwenye soko la pamoja ambapo laini kubwa ya kuunganisha Tanzania na Kenya kupitia Namanga imeshajengwa na imekamilika.
Amesema laini ya kuunganisha Tanzania na Zambia- TAZA imeshaanza kujengwa na itakamilika ifikapo 2026.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa sasa wa soko la pamoja la kuuziana umeme la nchi za kaskazini Mashariki EAPP na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini nchini Uganda . Dkt. Ruth Ssentamu amesema EAPP imeridhia ushiriki wa Makatibu Wakuu wa Nishati kutoka nchi wanachama kushirikishwa katika muundo wa kiutawala wa EAPP.
Amesema kuundo huo ni kwa ajili ya kusaidia kuchakata na kupitia taarifa kutoka kwa watendaji wa kisekta kabla ya kupelekwa katika kikao cha baraza la Mawaziri la nchi wanachama ili kutolewa maamuzi.
Aidha, Mhe Ssentamu amesema maadhimio hayo yamefikiwa kufuatia makubaliano ya mkutano wa 18 wa baraza la mawaziri ulioanyika nchini Kenya kuhusu umuhimu wa kupitia mapendekezo ya uendeshaji wa shughuli za EAPP.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba amesema pindi uuzaji wa umeme kwenye soko la pamoja utakapoanza utatoa nafasi za ajira kwa nchi wanachama wa EAPP pamoja na kubadilishana wataalamu hususan kwenye miradi ya kusafirisha umeme na kuiongezea TANESCO mapato.
Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo wa Baraza la Mawaziri wa Nishati uliongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dennis Londo, Katibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba.
Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mha. Gissima Nyamo-Hanga, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mipango, Utafiti na Uwekezaji TANESCO CPA Renata Ndege, viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.