Mwandishi wetu
ARUSHA: TAASISI zisizo za kiserikali nchini zimeiomba Serikali ya Tanzania kuzifanyia maboresho sheria ya Kupata taarifa ya mwaka 2016 na sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya mwaka 2002 ili kuondoa upungufu uliopo.
Meneja uchechemuzi wa Kituo cha sheria na haki za Binaadamu nchini(LHRC), Wakili Raymond Kanegene.akizungumza katika kikao kazi
cha kupitia sheria hizo ambacho kiliwashirikisha wadau kutoka serikalini na sekta binafsi amesema sheria hizo zinahitaji maboresho madogo ili ziwe bora zaidi.

Wakili Kanegene amesema kwa mujibu wa maoni ya wadau na utafiti uliofanywa na Taasisi ya kimataifa ya CIPESA unaonesha kuwa,katika ukanda wa nchi za Afrika ya Mashariki licha ya kila nchi kuwa na sheria zake ikiwepo sheria ya kupata taarifa lakini imebainika kila nchi sheria hiyo ina mapungufu. yake.
Amesema kwa mfano sheria ya kupata taarifa ya Tanzania kifungu cha 5(1) kinatoa haki za kila mtu kupata taarifa lakini 5(4) kinasema ambao wanaweza kupata taarifa lazima wawe raia wa Tanzania.
“kifungu kama hiki kinapaswa kitowe haki ya kila mtu kupata taarifa lakini kinaweza kuziweka taarifa katika makundi ni zipi anapaswa kupewa raia tu na taarifa zipi hapaswi kupewa mtu ambaye sio raia,” amesema.

Kanegene amesema uchambuzi wa sheria hiyo ya kupata taarifa kifungu cha 9 kinaeleza mtu ambaye anataomba taarifa atapewa taarifa hiyo sio zaidi ya siku 30 .
Amesema muda huo ni mrefu tofauti na sheria za nchi nyingine za Afrika Mashariki, ambapo Rwanda utapewa taarifa ndani ya siku 3 ,Kenya siku 21, Uganda siku 21 na Sudan Kusini siku 7.
“Mapendekezo ya wadau siku ziwe chache kwani mwandishi wa habari hawezi kusubiri kupata taarifa ndani ya siku 30 kwani taarifa inapaswa kutolewa kwa wakati,” amesema..
Akichambua sheria ya NGOs amesema pia ina upungufu ambao unaathiri sekta hiyo, miongoni mwa upungufu huo ni kutaka kila baada ya miaka 10 NGOS kupata usajili mpya, kuwepo sheria kali za kuzifunga ikiwepo kwa kushindwa kuwasilisha tu taarifa kwa taasisi zaidi ya tatu.
“lakini pia sheria hii imekuwa ikitaka kuwasilisha mikataba ya wahisani kabla ya kupata ufadhili lakini pia kutangaza kwenye vyombo vya habari taasisi inapopata zaidi ya sh 20 milioni mambo ambayo yanahitai maboresho”amesema
Amesema mapendekezo ni kuondolewa kifungu ambacho kinataka NGOs kusajiliwa upya kila baada ya miaka 10 ,kuwa na mfumo mmoja kutoa taarifa za utendaji na fedha wa NGOs ili taasisi zote ziweze kupata lakini pia kuwekwa utaratibu rafiki kutangaza miradi na mikataba yake.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya habari nchini(JOWUTA) Mussa Juma alisema maboresho ya sheria hizo yataongeza weledi katika.kufanya kazi na kuondoa migogoro isiyo ya lazima. Alisema sheria ya kupata taarifa bado haijatumika vizuri na wadau wengi hawaijuwi lakini ingekuwa nzuri ingesaidia sana kuondoa kuandokwa habari ambazo sio sahihi. ” kunapokuwa na urasimu.wa kupata taarifa ndipo taarifa potofu usambazwa hivyo ni muhimu kuwa na sheria rafiki kwa wadau”alisema
Mwenyekiti wa Taasisi ya habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA -TAN) Edwin Soko akichangia mjadala huo, alisema ni muhimu sheria kadhaa kuboreshwa kwendana na matakwa ya Katiba ya nchi na mikataba ya kimataifa.
“kuna taarifa nyeti ambazo kutolewa lazima kuwepo na utaratibu ikiwepo taarifa za masuala ya ulinzi na usalama na jambo hili hata katika maadili ya uandishi wa habari linajulikana”alisema
Amesema sheria ya kupata taarifa inaathiri wanahabari kwani l kwa mwandishi wa habari kuambiwa asubiri ndani ya siku 30 kupata taarifa ambayo anahitaji ni muda mrefu.
Mwenyekiti wa Kikosi kazi hicho, Sophia Komba akizungumza katika kikao hicho, alisema sheria nzuri ni zile ambazo zinasaidia ukuaji wa sekta husika na sio ambazo zinaathiri sekta husika.
Amesema sheria ya NGOs inahitaji maboresho makubwa ili kwendana na maoni ya wadau kwani sasa imekuwa ni tishio kwa sekta hiyo na kuanza kuathiri uendelevu wa mashirika mengi yasiyo ya kiserikali.
Ofisa Utetezi wa Mtandao wa Mashirika ya Watetezi wa Haki za Binaadamu nchini(THRDC) Paul Kisabo alisema sheria ya kupata taaria na sheria ya NGOs ni baadhi tu ya sheria ambazo zinahitaji maboresho kwa baadhi ya vifungu.
Wakili Kisabo amesema, binafsi amewahi kutumia sheria hiyo, kuomba taarifa katika taasisi ya Umma lakini kwa zaidi ya miezi sita sasa hajapata licha ya kufanya jitihada kubwa na hilo linawezekana kutokana na mapunguu ya sheria hiyo ya kupata taarifa.
Akifunga kikao hicho,Komba alitaka wadau walioshiriki kuendelea na majadiliano lakini pia kuongeza taasisi nyingine za serikali katika vikao vijavyo ili kuwa na uelewa wa pamoja wa sheria hizo na kujua mapungufu yake.
Kikao kazi hicho, kilichoandaliwa na LHRC ,kilishirikisha maofisa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo,Tume ya kurekebisha sheria, Chama.cha Mawakili.wa Tanganyika(TLS), Jumuiya ya kikristo Tanzania(CCT ) ,
Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania(JOWUTA), MISA- TAN, maofisa kutoka Wizara ya Sheria na Katiba, Wizara ya Maendeleio ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum,Baraza la Habari Tanzania(MCT) Jukwaa la wahariri(TEF) ,Jamii Afrika, na Mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali nchini.