Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 16

Serikali Yaanzisha Mkajati Mpya Wa Elimu Jumuishi

Na Lucy Ngowi

SERIKALI imezindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031 pamoja na miongozo tisa ya utekelezaji, hatua inayolenga kuondoa vikwazo vya elimu kwa wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalum nchini.

Sambamba na uzinduzi huo, Serikali imetoa vifaa saidizi vyenye thamani ya Sh. Milioni 730 kwa wanafunzi wenye ulemavu katika shule za sekondari na vyuo vikuu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha wanafunzi hao wanapata elimu bora.

Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali inaendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya elimu ili kupanua fursa za kujifunza, kuboresha mazingira ya kufundishia na kuandaa wananchi wenye maarifa na ujuzi unaohitajika katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Habari Picha 14164

Amesema katika kuimarisha elimu jumuishi, watumishi 2,058 wamepatiwa mafunzo, wakiwemo walimu wa elimu maalum 1,276, walimu wenye ulemavu 242 na walezi 346.

Aidha, Serikali imechapisha na kusambaza vitabu 22,600 vya Breli na vitabu 850,000 vyenye maandishi yaliyokuzwa kwa ajili ya wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu, ili kuwawezesha kupata nyenzo zinazokidhi mahitaji yao ya kujifunza.

Profesa Mkenda amesema Serikali pia imeifanya Lugha ya Alama ya Tanzania kuwa somo la lazima kwa walimu tarajali, huku walimu tarajali 2,000 wakifadhiliwa kusomea shahada ya elimu maalum.

Habari Picha 14165

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema miongozo tisa iliyozinduliwa inahusu maeneo mbalimbali, yakiwemo mafunzo kazini, michezo, teknolojia saidizi, elimu ya awali, Lugha ya Alama ya Tanzania na lugha ya alama mguso.

Amesema miongozo hiyo inalenga kuondoa vikwazo vya kimazingira, mawasiliano na kiteknolojia vinavyoweza kuwazuia wanafunzi wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kujifunza.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Juma Sekiboko, amesisitiza umuhimu wa walimu na wanafunzi kutumia kwa usahihi vifaa saidizi vinavyotolewa ili viweze kusaidia kuboresha ujifunzaji.

Mkakati huo unalenga kuimarisha mfumo wa elimu jumuishi nchini kwa kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu na mahitaji maalum wanapata fursa sawa za elimu na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujifunza.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.